WAZIRI MAVUNDE AKEMEA MITOBOZANO MIRERANI - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Sunday 19 November 2023

WAZIRI MAVUNDE AKEMEA MITOBOZANO MIRERANI

 



Na Mwandishi wetu, Mirerani


maipacarusha20@gmail.com


WAZIRI wa Madini, Anthony Peter Mavunde amepiga marufuku wachimbaji wa madini ya Tanzanite mji mdogo wa Mirerani, wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, wanaochimba na kutoboa kwenye migodi mingine chini ya ardhi kwa makusudi na kusababisha migogoro, uhasama na vifo.


Waziri Mavunde ameyasema hayo wakati akizungumza na wadau wa madini ya Tanzanite, mji mdogo wa Mirerani, wilayani Simanjiro, mkoani Manyara, kwenye ziara yake ya siku moja.


Amesema suala la kudai kuwa chini mgodini hakuna mpaka siyo sahihi kwani chini kuna mpaka hivyo kila mchimbaji madini wa madini ya Tanzanite, anapaswa kufanya shughuli zake kwenye eneo lake.


Amesema Serikali haitamvumilia mtu yeyote atakayekwenda kinyume kwa kuchimba kwenye eneo la mwenzake hivyo wachimbaji wa madini ya Tanzanite wazingatie hilo.   


“Tunapaswa kufuata utii wa sheria, kanuni, taratibu na miongozo ya madini ya Tanzanite ili kuwepo na tija ya uchimbaji madini, usalama na amani na siyo vinginevyo,” amesema Waziri Mavunde.


Hata hivyo, amemuagiza ofisa madini mkazi (RMO) wa Mirerani Chacha kuhakikisha kuwa anasuluhisha migogoro ya mitobozano ya migodi ya madini ya Tanzanite ili shughuli zifanyike kwa usalama.


“Mimi siyo waziri wa mitobozano hivyo mnapaswa kumaliza ninyi wenyewe kwani mimi naongoza sekta ya madini pote nchini siyo Mirerani pekee ila nakupongeza RMO Chacha Marwa umeanza vizuri kwa kuwakutanisha waliotobozana,” amesema Mavunde.


Meneja mkuu wa kampuni ya Franone Mining LTD, Vitus Ndakize, inayochimba madini ya Tanzanite kitalu C, amesema miongoni mwa changamoto wanazopitia ni mitobozano na wachimbaji ikiwemo migodi ya kampuni ya Tanzanite Explorer na Gem & Rock.


Ndakize amesema baadhi ya wamiliki wa migodi iliyopo kitalu D na kitalu B ‘Opec’ wamekuwa na dhana potofu kuwa madini yapo mkondo wa kitalu C pekee jambao ambalo siyo sahihi.


Amesema wao kama Franone Mining LTD, wapo tayari kutoa utaalam wa kijiolojia kwenye baadhi ya migodi itakayohitaji ili waweze kupata njia zinazotoa madini na siyo kudhani suluhisho ni kutobozana na kitalu  C.


Hata hivyo, mkurugenzi wa kampuni ya Tanzanite Explorer LTD, Lenganasa Soipei amesema suala la kuwepo mitobozano halikwepeki kutokana na jiolojia ya madini ya Tanzanite inavyokwenda mshazari wakati wa uchimbaji wake.


“Tumekaa kikao hivi karibuni kupitia RMO Chacha na tukakubaliana kila mmoja achimbe kwenye njia yake ili kuwepo na usalama kwani kila mtu ametumia gharama nyingi katika kuchimba,” amesema Lenganasa.

 


No comments: