DCEA Kanda ya Kaskazini yatoa Elimu kwa Waraibu Jijini Arusha - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Monday, 4 December 2023

DCEA Kanda ya Kaskazini yatoa Elimu kwa Waraibu Jijini Arusha

 





Na Prisca Libaga Maelezo Arusha


maipacarusha20@gmail.com


WARAIBU zaidi ya 150 Kanda ya Kaskazini Jijini Arusha wamepatiwa Elimu juu ya madhara ya matumizi ya dawa za kulevya na kutakiwa kuacha kuendelea kutumia dawa hizo zilizobainika kupoteza nguvu kazi ya taifa.


Mafunzo hayo ni mwendelezo wa mafunzo mbalimbali yanayotolewa katika maeneo tofauti tofauti nchini na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) katika Kanda ya Kaskazini yamefanyika chuo cha ufundi Arusha (ATC) Jijini Arusha


Ofisa Msimamizi wa Elimu kutoka Mamlaka hiyo Kanda ya Kaskazini (DCEA)Shaban Miraji alisema lengo hasa la mafunzo hayo ni kudhibiti matumizi ya dawa za kulevya hapa nchini na kuwaasa waraibu hao kutoendelea kujihusisha katika janga hilo hatari.


"Elimu hii tumeileta kwenu kutokana na mikoa ya Kanda ya Kaskazini ambayo ni Arusha, Kilimanjaro,Tanga na Manyara kuonekana kuwa miongoni kwa mikoa inayoongoza kwa matumizi ya dawa za kulevya aina ya bangi na Mirungi" alisema.


Aidha alieleza kuwa,katika kipindi cha miezi miwili (September na November, 2023)Mamlaka hiyo imefanikiwa kukamata bangi kavu zaidi ya gunia 237 pamoja na mbegu zake kilo 210 pia kiasi kikubwa cha mirungi na heroini kwenye operesheni iliyofanyika katika ya Kanda ya Kaskazini.


"Mamlaka imefanikiwa kutoa elimu katika jamii pamoja na vyuoni, Shule za msingi na Sekondari kwa lengo la kuwandaa wanafunzi kutojihushisha na matumizi ya dawa hizo" alisema Shaban.


Katika hatua nyingine alisema mamlaka(DCEA) imebaini baadhi yao katika kanda hiyo hawajaanza kujitokeza kupata matibabu na Serikali imejitahidi kusogeza huduma kutokana na kanda hiyo kuwa na vituo viwili ambavyo kimoja kipo Jijini Arusha na Kingine kipo Jijini Tanga.


"kuna vituo 16 hapa nchini, nyumba za kuhudumia warahibu zaidi ya 53 na kwa Kanda ya Kaskazini pekee zipo nyumba 24" alisema Shaban.


Alisema, Mamlaka hiyo imejipanga kuendelea kutoa Elimu kwa kutumia majukwaa mbalimbali ikiwemo sekta ya sanaa hapa nchini ambao wameonekana ndio kundi kubwa linalowafikia vijana kwa haraka"wale waliobanika kuwa na vipaji tutawaendeleza ili waweze kuachana na matumizi ya dawa hizo".

"Tumebaini kuwa Dawa za kemikali zinaharibu meno kwa kuozesha na watumiaji wa mirungi wanaua Ini, hivyo nitoe Rai kwa watumiaji wa mirungi kuacha, hususani madereva wa masafa marefu(Lori) kwani utumiaji wake unachangia ongezeko la wagonjwa Bawasiri"alisema Shaban.


Naomi Massawe ambaye ni miongoni mwa Waraibu waliopata mafunzo alieleza kuwa alianza kutumia dawa za kulevya kwa kipindi cha miaka mitano nyuma pindi alipokuwa akijishughulisha na kazi ya uchimbaji madini katika mji mdogo wa Mirerani.

 

"Kwa sasa nina miaka miwili toka kuacha kutumia dawa hizo, najihusisha na masuala ya ususi lakini changamoto nikisuka napewa pesa kidogo ambayo haikidhi mahitaji yangu, niliacha dawa hizi baada ya mtoto wangu kutoridhika na matendo yangu lakini pia nitambua hazina faida kwenye maisha yangu"alisema Naomi.


Mkuu wa Idara ya Afya na Kitengo cha Dawa ya Methodone katika Hospitali ya Rufani Mkoa wa Arusha Mountmeru Dkt Said Salum alifafanua kuwa huduma za matibabu kwa waraibu wa dawa za kulevya ni bure hivyo aliwataka kufika katika vituo vilivyopo mkoani hapo ilikuweza kupatiwa matibabu.


DCEA Kanda ya Kaskazini imetoa mafunzo hayo kwa kushirikana na Asasi mbalimbali kama vile Kimara Peer, Care for All, YOVARIBE, YCR, Mount MERU Sober House, Ofisi ya Ustawi wa Jamii Arusha, Ofisi ya Mganga Mkuu Arusha , Mratibu wa Afya ya Akili Arusha, Msimamizi wa Mountmeru Clinic pamoja na Vyombo vya Habari.







No comments: