FRANONE WAACHWE WAFANYE KAZI - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Friday 29 December 2023

FRANONE WAACHWE WAFANYE KAZI

 





Na: Joseph Lyimo, Mirerani 


maipacarusha20@gmail.com


KAMPUNI ya Franone Mining LTD inayomiliki kitalu C kwa asilimia 84 na Serikali asilimia 16 ipo kihalali kwenye eneo hilo baada ya kushinda tenda ya kuchimba madini ya Tanzanite Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara.


Wamiliki wake Onesmo Mbise, Francis Matunda na Vitus Ndakize wanamiliki kitalu C kwa kufanya kazi kihalali bila kumuonea mtu, hivyo wanapaswa kuungwa mkono na siyo kulaumiwa juu ya eneo la kitalu C.


Hivi karibuni Waziri wa Madini, Antony Mavunde alitembea machimbo ya madini ya Tanzanite mji mdogo wa Mirerani na kuzungumza na wachimbaji wa madini hayo na kutoa maagizo kadhaa.


Waziri Mavunde aliwaeleza wachimbaji madini ya Tanzanite, kuwa yeye siyo waziri wa mitobozano, hivyo wafanye kazi zao, ili mradi hawavunji sheria zilizopo kwa kuzifuata.


Waziri huyo akaeleza kuwa wachimbaji madini ya Tanzanite wanapaswa kufanya shughuli zao kwa kufuata sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa na siyo vinginevyo.


Hivi karibuni, baadhi ya wamiliki wa migodi, wachimbaji wa kitalu B (Opec) na kitalu D, walikuwa wakilalamika juu ya mwekezaji wa kitalu C kampuni ya Franone Mining LTD kuwa wanawazuia kuchimba kwenye maeneo yao jambo ambalo siyo sahihi.


Wamekuwa wakidai kuwa wanarudishwa nyuma baada ya kuingia kwa chini kwenye njia ya mgodi wa Franone jambo ambalo siyo makosa kwani mtu akiingia kwenye eneo la mwenzake anapaswa kurudishwa nyuma.


Eneo la kitalu C la mwekezaji kampuni ya Franone Mining lipo kihalali hivyo wachimbaji wanaoizunguka kampuni hiyo wanapaswa kufanya shughuli zao bila kuwalalamikia wenzao.


Kitalu C kinamilikiwa na Serikali kwa asilimia 16 na kampuni ya Franone Mining LTD chini ya wamiliki wake, Onesmo Mbise, Francis Matunda na Vitus Ndakize, wanamiliki asilimia 84 zilizobaki.


Kutokana na kuwa kihalali kwenye eneo hilo la kitalu C, kampuni ya Franone inapaswa kuachiwa nafasi na kufanya kazi kwani hii ni kampuni ya watanzania halisi na siyo kama zile kampuni za awali ambazo zilikuwa na migogoro na manyanyaso ya kila mara kwa wachimbaji wadogo.


Wachimbaji wadogo wa madini ya Tanzanite wanapaswa kutambua kuwa kampuni ya Franone Mining LTD inashirikiana na serikali katika kuchimba madini kitalu C.


Pamoja na kuchimba madini ya Tanzanite tumeshuhudia kampuni ya Franone Mining LTD imekuwa ikisaidia jamii inayowazunguka kwenye wilaya ya Simanjiro ili kurejesha kwa jamii kile wanachokipata.


Hivi karibuni kampuni ya Franone Mining LTD ilitoa msaada wa chakula kwa wanafunzi wa shule za msingi Naisinyai na Oloshonyokie baada ya eneo la Naisinyai kukumbwa na ukame hivyo wazazi na walezi kushindwa kuchangia chakula mashuleni 


Pia hivi karibuni kulitokea mafuriko kwenye kata za Shambarai na Msitu wa Tembo na kampuni hiyo ikajitolea msaada wa chakula cha thamani ya sh 31 milioni na kugawa kwa waliokumbwa na maafa hayo.


Franone imetengeneza ajira rasmi 328 wakiwemo wataalamu 30 na kutoa ajira zisizo rasmi zaidi ya 1,000 ikiwemo mama na baba lishe, madereva wa kubeba abiria (bodaboda), wauza matunda na wajasiriamali wengineo.


Tangu mwaka 2022 kampuni ya Franone Mining LTD iliposhinda zabuni ya kuchimba madini ya Tanzanite kitalu C, imefanya kazi kubwa ya kukarabati miundombinu ya mgodi mkubwa wa Main Shaft ambayo inafanya kazi na kupata uzalishaji.


Tangu wakati huo baadhi ya wachimbaji wa madini ya Tanzanite waliopo jirani na Franone wanaochimba kitalu B na D wamekuwa wakitaka kuruhusiwa kuingia kwenye eneo lisilo lao kupitia chini mgodini.


Wachimbaji hao wamekuwa wakilalamika mithili ya kuwa wana haki ya kuingia na kufanya kazi chini mgodini ndani ya mgodi wa mwekezaji Franone Mining LTD.


Kabla ya Franone kushinda zabuni ya uchimbaji wa madini kitalu C, Rais Samia Suluhu Hassan aliahidi kuwa kitalu hicho kitalindwa kwani serikali ina maslahi nacho.


Pamoja na serikali kuwa na hisa asilimia 16 kwenye kitalu C pia serikali inapata kodi kupitia kodi ya ajira na kodi ya madini yanayozalishwa na kampuni ya Franone Mining LTD kupitia mgodi wao.


Tunatarajia kampuni ya Franone Mining LTD itaachiwa ifanye kazi zake kwa uhuru na amani na siyo siasa chafu kuingizwa na kutupiwa lawama ili hali wanachimba kwenye kitalu walichokabidhiwa na serikali baada ya kushinda zabuni.


Hivi karibuni ofisa madini mkazi RMO Mirerani Nchagwa Chacha Marwa ameelezea wazi kuwa Franone Mining LTD haipaswi kulalamikiwa kwani eneo la kitalu C wamemilikishwa kihalali na wapo kisheria.


No comments: