Mtuhumiwa wa ujangili afungwa miaka 20 jela - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Thursday 18 January 2024

Mtuhumiwa wa ujangili afungwa miaka 20 jela

 



Na: Andrea Ngobole, Maipac 


maipacarusha20@gmail.com


Mtuhumiwa sugu wa ujangili,Said Magodoro amefungwa miaka 20 Jela na Mahakama ya Hakimu Mkazi wilaya Babati kutokana na kujihusisha na matukio ya ujangili na kukamatwa na Nyara za serikali.


Magodoro alikamatwa pamoja na wenzake watatu  na vipande sita vya meno ya Tembo.


Mtuhumiwa huyo kabla ya kukamatwa alikuwa akisakwa kwa muda mrefu kwa tuhuma za ujangili katika eneo la hifadhi ya Jamii ya wanyamapori ya Burunge na maeneo ya jirani na hifadhi ya Taifa ya Tarangire.


Hakimu Mkazi wilaya Babati, Twahir Mushi akisoma hukumu hiyo Jana amesema mtuhumiwa huyo,anatiwa hatiani kwa kosa la kukamatwa na Nyara za serikali kinyume cha sheria.


Alisema mtuhumiwa huyo alikamatwa na vipande sita vya meno ya Tembo julai 4, mwaka 2023 wilayani Babati mkoa wa Manyara.


Alisema ushahidi ambao umetolewa Mahakamani umemtia hatiani Magodoro huku Watuhumiwa wengine wawili wakiachiwa huru.


Watuhumiwa walioachiwa huru ni lssa Hussein na Juma Mohamed baada ya kukosekana ushahidi wa kuwatia hatiani.


Awali, Waendesha mashitaka wa Mamlaka ya Usimamizi wanyamapori nchini(TAWA) Getrude Kariongi na Shahidu Kajwangya walieleza Mahakama kwa mtuhumiwa huyo amekuwa akijihusisha kwa ujangili kwa muda mrefu.


Kariongi alisema kabla ya kosa ambalo limemfikisha Mahakamani mtuhumiwa huyo,tayari alikuwa amefungwa kwa kosa la kukamatwa na Nyama ya Pundamilia.


"Kosa hili mtuhumiwa alitenda wakati yupo nje ya dhamana katika kesi nyingine ya ujangili ambayo ilikuwa inamkabili"alisema


Alisema mtuhumiwa huyo  alikuwa anatuhumiwa kujihusisha na ujangili katika maeneo ya hifadhi ya Jamii ya Burunge (Burunge WMA)na jirani na  maeneo ya hifadhi za Taifa za Tarangire na hifadhi ya Manyara.


"Mheshimiwa Hakimu mtuhumiwa huyo anatumikia kifungo Kingine cha miaka 20 kutokana na kujihusisha na ujangili na alitenda kosa hili akiwa nje ya dhamana tunaomba apate adhabu kali kwa kuwa anahujumu uchumi wa Taifa"alisema.


Hata hivyo, baada ya mtuhumiwa kupewa muda wa kujitetea baada ya kutiwa hatiani aliomba Mahakama kumpunguzia adhabu kwani ana familia ambayo inamtegemea.


Hata hivyo, licha ya maelezo hayo ya mtuhumiwa huyo,Hakimu Mushi alimuhukumu kifungo cha miaka 20 jela na kuamuru vipande sita vya meno ya Tembo vikabidhiwe kwa Mkurugenzi wa Wanyamapori nchini.


Kukamatwa na kufungwa kwa mtuhumiwa huyo ni jitihada za pamoja baina ya TAWA,TANAPA, Burunge WMA na Taasisi ya chem chem association ambayo imeweka shughuli za Utalii katika eneo la Burunge WMA.


Kikosi Maalum ya Kupambana na ujangili kimeundwa katika eneo hilo la Ikolojia ya Tarangire na Manyara ambapo zaidi ya million 400 zimekuwa zikitolewa na chemchem kila mwaka Kupambana na ujangili .


Licha ya kuundwa kikosi hicho mafunzo ya matumizi ya Teknolojia za kisasa yamekuwa yakitolewa kwa askari wa Wanyamapori lakini pia jinsi ya kupeleleza na kukamata na kutunza vielelezo vya Watuhumiwa wa ujangili. 



No comments: