Wapagazi Mlima Kilimanjaro na Meru Sasa kulipwa 25,000 Kwa Siku - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Saturday 6 January 2024

Wapagazi Mlima Kilimanjaro na Meru Sasa kulipwa 25,000 Kwa Siku


Mwenyekiti wa Umoja wa vyama vya wapagazi nchini, Loshiye Mollel akizungumza katika mkutano Mkuu huo

Katibu Mtendaji wa chama Cha wamiliki wa Kampuni za Utalii (TATO)Sirili Akko,



Na Mwandishi wetu, Kilimanjaro.


maipacarusha20@gmail.com


Hatimaye Malipo ya Wasaidizi wa Watalii wanaopanda Mlima Kilimanjaro na Meru  (Wapagazi),yametangazwa kupanda kutoka sh 15,000 kwa siku hadi sh 25,000 kwa siku kuanzia January mosi mwaka huu tangazo ambalo limepokelewa kwa shangwe kubwa na wapagazi.


Kwa Wastani wapagazi hupanda Mlima Kilimanjaro na kushuka kati ya siku tano hadi 10 ,huku Mlima Meru hupanda kwa kati ya siku 3 hadi 4.


Malipo yanatarajiwa kuongezeka tena mwakani kuanzia January mosi mwaka 2025 na kufikia sh 35,000 kwa siku.


Maamuzi ya kupandishwa malipo hayo, yametangazwa leo Januari 3,2024 katika mkutano uliowashirikisha wamiliki wa Kampuni za Utalii vyama vya wapagazi na viongozi kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii na Wizara ya Kazi,uliofanyika ukumbi wa Uhuru Moshi ,mkoani Kilimanjaro.


Mwenyekiti wa Umoja wa vyama vya wapagazi nchini, Loshiye Mollel amesema tangu mwaka 2008 wamekuwa na maombi ya kupanda kwa malipo ya wapangazi lakini walikwama.


"Mwaka 2008 serikali kupitia Waziri wa Maliasili ilitoa Tangazo la Serikali namba 228 ya kupandisha malipo kutoka 8000 hadi 20,000 hata hivyo haijawahi kutekelezwa ila mwaka huu sasa tumefikia makubaliano"amesema


Alisema vyama vya wapagazi vikiongozwa chama Cha wapagazi Tanzania (TPO) viliendelea na Vikao vya maombi ya kupanda malipo hadi kufikisha Kamati za Bunge na Wizara ya Kazi na Mamlaka nyingine za serikali.


Mollel amesema baada ya majadiliano ya muda mrefu hatimaye Desemba 29,mwaka Jana walifikia makubaliano katika kikao kilichoitishwa na Wizara ya Maliasili na Utalii, kushirikiana na Kamishna wa kazi,Mamlaka ya Kodi ya Mapato (TRA) na vyombo vingine.


Akizungumza katika kikao hicho, Katibu Mtendaji wa chama Cha wamiliki wa Kampuni za Utalii (TATO) Sirili Akko, amesema wamekubaliana nyongeza ya malipo hayo ili kukuza sekta ya Utalii nchini.


Akko amesema, kuanzia January mosi malipo yatakuwa dola 10 kwa siku ambazo ni sh 25,000 kwa siku na kuanzia  January mwaka 2025 itakuwa dola 15 ambazo ni sh 35,000.


"Sisi kama TATO tayari tumekubaliana hili na jambo hili Waziri mwenye dhamana na serikali wanalifatilia sana ili kumaliza mgogoro huu wa muda mrefu"amesema.


Amesema ili kufanikisha malipo hayo wamekubaliana wapagazi wote lazima wawe na namba ya mlipakodi(TIN) na akaunti benki ili fedha zao ziwe zinalipwa moja kwa moja benki la kampuni za utalii.


Afisa Utalii Kanda ya Kaskazini, Franklin Alexander alisema Wizara ya Maliasili na Utalii itahakikisha makubaliano hayo yanafikiwa.


Alexander anesema, Kampuni zote za Utalii zitapaswa kutekelezwa maamuzi hayo na Wizara itasimamia na ambao watapuuza hatua zitachukuliwa.


Mpagazi Kolokolo Omar Kolokolo alipongeza serikali na Rais Samia Suluhu kwa kuwezesha maboresho ya malipo yao kwani kwa miaka 15 wamekuwa wakihangaika.


"Leo ni kama siku yetu ya mahafari, tunamshukuru sana Rais Samia na Waziri wetu wa Maliasili na Utalii, hiki kilikuwa kilio kikubwa sana kwetu Sasa kimeisha"amesema.


Kuna wapagazi 16,640 ambao hufanyakazi katika mlima Kilimanjaro na Meru.



No comments: