Mwiba Holding Ltd , TANAPA ,wapongezwa kudhamini Tamasha la Utalii Same, Idadi ya Watalii yavunja rekodi - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Monday 26 February 2024

Mwiba Holding Ltd , TANAPA ,wapongezwa kudhamini Tamasha la Utalii Same, Idadi ya Watalii yavunja rekodi

 


Gertrude Nyangaka mwakilishi wa kampuni ya Mwiba Holding akizungumza katika tamasha la Same Utalii festival 



      

Waziri wa Maliasili na Utalii Angellah Kairuki kulia akiwa katika tamasha la Same Utalii festival 

Mwandishi wetu,Same


maipacarusha20@gmail.com


Kampuni ya Utalii ya Mwiba Holding Ltd na Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) ,wamepongezwa kwa kujitokeza kudhamini Tamasha la Utalii la Same, mkoani Kilimanjaro.


Tamasha hilo la aina yake  lililowavutia maelfu ya watu,mgeni rasmi alikuwa ni Waziri wa Maliasili na Utalii, Angellah Kairuki ambaye alipongeza kampuni ya Mwiba, Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA), Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA)Bodi ya Utalii na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori nchini (TAWA) na Taasisi nyingine za fedha na simu kwa kudhamini Tamasha hilo.


Akizungumza katika Tamasha hilo, Waziri Kairuki alipongeza Uongozi wa Serikali wilaya ya Same kwa kuandaa Tamasha hilo,ambalo limeweza kubainisha vivutio kadhaa vya Utalii ambavyo vinapatikana wilayani Same.


Waziri Kairuki alisema miongoni mwa vivutio ambavyo vinapatikana Same ni pamoja  Hifadhi ya Taifa ya mkomazi, Msitu Chome, Shengena ambapo kuna ndege wa kipekee wanapatikana eneo hilo pekee Duniani pia kuna mapango ya kuvutia.


"Lakini pia hapa Same yamebainishwa maeneo 13 ya Mali kale ambayo ni kivutio cha watalii, nawapongeza sana viongozi wa Same kwa Tamasha hili ambalo pia limewashirikisha wajasiriamali na vikundi vya wanawake na vijana"alisema 


Alisema Tamasha hilo ni utekelezwaji wa llani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020/25 Ibara ya 67, kuwa ifikapo mwaka 2025 Tanzania imepokea watalii million 5 na fedha zaidi ya trilioni15.


Alisema hadi sasa idadi ya watalii inaendelea kuongezeka kwani kuanzia January 2023 hadi Novemba 2023 watalii walioingia nchini walikuwa ni 1,808,205 ambapo mwaka 2022 watalii walikuwa ni 1,400,000 tu.


"Kwa takwimu za Benki kuu tunatarajia watalii kuwa wameongezeka zaidi Hadi kufikia Mwezi huu"alisema.


Akizungumza katika Tamasha Hilo kwa niaba ya Kampuni ya Mwiba Holding Ltd, Meneja Masoko Afrika Mashariki, Gertrude Nyangaka alisema Tamasha hilo limekuwa na mafanikio makubwa.


Nyangaka alisema Mwiba Holding Ltd inaunga mkono jitihada za kuendeleza uhifadhi na Utalii nchini, kutunza mazingira na kuendeleza utamaduni na Urithi wa Taifa.


Kamishna wa uhifadhi wa TANAPA, Juma Kuji alisema Tamasha hilo limeweza kuvutia watalii na wawekezaji na TANAPA itaendelea kushirikiana na wadau wa sekta ya Utalii kuvutia watalii na uwekezaji.


Akizungumza katika Tamasha hilo, Kaimu Mkuu wa mkoa Kilimanjaro Abdalah Mwaipaya na Mkuu wa wilaya Same, Kasilda Mgeni walieleza Tamasha litakuwa likifanyika kila mwaka.


Mwaipaya ambaye ni Mkuu wa wilaya ya Mwanga, alisema Tamasha lijalo watashirikiana na Same ili kuliboresha zaidi Tamasha hilo na kuvutia watalii zaidi.


Kwa Upande wake Kasilda licha ya kupongeza wafadhili pia alipongeza kamati ya maandalizi ya tamasha hilo na viongozi wote wa mkoa na Taasisi mbalimbali ikiwepo benki ya NMB Kampuni ya simu ya Tigo na nyingine nyingi kwa kufanikisha Tamasha hilo.



No comments: