Mkurugenzi Mkuu TAWIRI, Dk Eblate Ernest Mjingo akifafanua jambo Kwa waandishi wa Habari |
Na: Mwandishi wetu, maipac
maipacarusha20@gmail.com
Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori nchini (TAWIRI) imebainisha kwa vitendo Matumizi ya teknolojia Katika Uhifadhi wa Wanyamapori yalivyo na tija katika uhifadhi endelevu.
Akizungumza na waandishi wa habari, Mkurugenzi Mkuu TAWIRI, Dk Eblate Ernest Mjingo amesema teknolojia mbalimbali zimerahisisha tafiti za wanyamapori nchini kufanyika kwa wakati na kwa usahihi zaidi.
Dk. Mjingo amebainisha miongoni mwa teknolojia zinazotumika katika tafiti za wanyamapori ni pamoja na matumizi ya teknolojia ya akili mnemba (artificial intelligence) kuchakata takwimu na uchambuzi wa picha katika zoezi la kuidadi wanyama (sensa), teknolojia ya mikanda ya visukuma mawimbi( GPS satellite Collar) kufuatilia mienendo ya wanyamapori, matumizi ya ndege zisizo na Rubani rubani (Drone) kutatua changamoto ya wanyamapori wakali na waharibifu .
Pia, matumizi ya helikopta/ndege kuwafuatilia wanyamapori kwa matibabu au kuwarejesha wanyama maeneo ya hifadhi, kamera za kutega (camera trap) kubaini aina ya wanyamapori waliopo katika maeneo mbalimbali na changamoto za uhifadhi na tekinolojia ya vinasaba (DNA) kutambua afya ya uzazi wa wanyamapori kwenye mifumo ikolojia mbalimbali.
Dk.Mjingo amesema awali kabla ya matumizi ya teknolojia kulikuwa na ugumu katika kufanya tafiti za wanyamapori baadhi ya maeneo kwani iliwalazimu watafiti kutumia muda mrefu kufanya tafiti, kutumia gharama kubwa, usalama mdogo .
" Kwa kutumia teknolojia ya Akili mnemba (AI) kuchambua picha na kuchakata takwimu imesaidia kutumia nusu ya siku zilizokuwa zinatumika awali sambamba na kupunguza gharama " ameeleza Dkt. Mjingo
Dk. Mjingo amebainisha awali ilikuwa vigumu kufuatlia tabia za wanyamapori kwani wanyamapori wakiona gari au watu mara nyingi hubadili tabia sambamba na ugumu kufuatilia wanyamapori nyakati za usiku, msimu wa mvua na maeneo yasiyofikika ambapo kwa sasa teknolojia ya kamera za kutega (camera trap) inatumika nyakati za mchana na usiku.
Ametoa wito kwa wadau wa uhifadhi na utalii ndani na nje ya nchi kushirikiana na TAWIRI kwa kuzingatia tafiti za wanyamapori ni muhimu katika sekta ya uhifadhi na utalii nchini ambapo pia ametoa wito kwa mamlaka za uhifadhi kutumia ushauri wa kisayansi unaotokana na matokeo ya tafiti mbalimbali.
Maadhimisho ya siku ya wanyamapori kitaifa yamefanyika wilayani Babati mkoa Manyara ambapo mgeni Rasmi alikuwa Waziri wa Maliasili na Utalii.
Katika maadhimisho hayo Angellah Kairuki pia ameelezea mikakati ya Wizara yake kuendeleza uhifadhi kwa kujumuisha Teknolojia za kisasa.
Katika utekelezwaji wa Mpango wa matumizi ya Teknolojia za kisasa katika uhifadhi tayari viongozi wa jumuiya ya hifadhi ya Jamii Burunge walipelekwa Ikona WMA kujifunza matumizi ya Technolojia za kisasa kuzuiwa migogoro baina ya Binaadamu na wanyamapori
Katika ziara hiyo ya mafunzo ambayo ilidhaminiwa na Taasisi ya chemchem foundation, viongozi hao wa WMA walipata elimu juu ya matumizi ya nyaya za umeme kuzuiwa wanyamapori wakali na waharibifu kuingia katika makazi ya watu na kufanya uharibifu wa mazao na kusababisha vifo.
Ikona WMA kwa kushirikiana na Taasisi ya Grumet imeweza kupunguza migogoro baina ya wanyamapori na Binaadamu kutokana na kuweka uzio wa umeme kutenga maeneo yaliyohifadhiwa na maeneo ya kijamii
Ziara ya mafunzo hayo pia ikimshirikisha Mkurugenzi wa Halmashauri ya Babati Anna Mbogo, Maafisa wanyamapori wa mkoa Manyara na Babati ambao wote walijiridhisha umuhimu wa matumizi ya Teknolojia za kisasa katika uhifadhi.
Meneja wa Chemchem, Clever Zulu alisema ziara hiyo imekuwa na manufaa makubwa na wanatarajiwa mafunzo zaidi kutolewa kwa viongozi wa Burunge WMA kuweza kupunguza migogoro baina ya wanyamapori na Binaadamu.
Katibu wa Burunge WMA, Benson Mwaise pia alisema Uongozi wake pia utaandaa ziara nyingine Ikona WMA kujifunza zaidi juu ya utatuzi wa migogoro baina ya wanyamapori na Binaadamu na kuwa na Uhifadhi endelevu
No comments:
Post a Comment