Na Lilian Lucas, Morogoro
maipacarusha20@gmail.com
WAZIRI wa Viwanda na Biashara Dk Ashatu Kijaji amesema wizara kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa sekta ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara imeendelea kuboresha mazingira ya kuanzisha na kufanya biashara, uwekezaji na uendelezaji wa viwanda, kwa kuweka mifumo yenye tija ili kuchochea mageuzi ya sekta hizo.
Alisema hayo mjini Morogoro wakati wa kikao kazi kati yake na wakuu wa idara ya Viwanda, Biashara na UWEKEZAJI kutoka mikoa 26.
Dk Kijaji alisema mifumo hiyo Ina nia ya kuleta maendeleo jumuishi na endelevu kwa kutumia rasilimali zilizopo na kuzingatia umuhimu wa sekta katika kukuza uchumi na kuongeza fursa za ajira.
Alitaja baadhi ya mifumo kuwa ni pamoja na Mfumo wa Ufuatiliaji na Tathimini, Mfumo wa Ukusanyaji Mapato, Mifumo ya sajili za kibiashara na ya Utoaji wa Leseni.
"Muundo uliopitishwa mwaka 2022 na Mwongozo uliotolewa umeainisha majukumu ya Idara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji katika Sekretariati za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa (LGAs) katika kusimamia maendeleo ya viwanda, biashara na uwekezaji kupitia Sera na Mikakati mbalimbali inayosimamia sekta hizo nchini," alisema.
Waziri huyo alisema matarajio yake na Serikali ni kuwa Mwongozo huu utaongeza ufanisi na kuleta ustawi wa sekta za viwanda, biashara na uwekezaji pamoja na kuchochea maendeleo ya ukuaji wa uchumi nchini.
Alisema Mwongozo huo una lengo la kujenga uelewa wa pamoja na misingi ya utekelezaji wa majukumu ya idara ya viwanda, biashara na uwekezaji ili kuwa na mazingira bora na shindani ya uwekezaji na ukuaji shirikishi, kutafsiri kwa vitendo,uwepo wa idara hiyo katika Mikoa na Halmashauri ili kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu ya Watalaam wa Biashara wanaohudumia sekta ya hiyo kwenye Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa.
Pia Waziri Dk Kijaji alisema Serikali imedhamilia kuboresha na kuimarisha mazingira ya biashara nchini ili kuendana na azma ya kufanya mageuzi ya kiuchumi na viwanda kwa ajili ya kuleta maendeleo endelevu ya jamii.
Alisema juhudi zimekuwa zikifanyika na Serikali hususani Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni(BRELA) ya kutoa mafunzo kwa Maafisa Biashara kuhusu Sheria ya Leseni za Biashara Sura 208, Sheria ya Taifa ya Usajili na Leseni za Viwanda Sura ya 46 na shughuli za Sajili mbalimbali zinazofanywa na BRELA.
Afisa Mtendaji Mkuu wa Brela Godfrey Nyaisa alisema lengo kuu la kikao kazi hicho ni kuwajengea uelewa Wakuu wa Sehemu na Idara za Viwanda, Biashara na Uwekezaji kutoka katika Mamlaka za Mikoa na Serikali za Mitaa kuhusu Sheria, Kanuni na Taratibu za sajili na utoaji wa leseni zinazosimamiwa na BRELA na namna ambavyo wanaweza kushirikiana katika kutekeleza majukumu ya kukuza sekta ya biashara na uwekezaji nchini.
Alisemq Brela inaendelea na uboreshaji wa utoaji wa huduma zake na kuweka mazingira wezeshi ya biashara nchini ambapo kwa sasa huduma zote za Brela zinapatikana kwa njia ya mtandao kupitia mifumo ya Online Registration System (ORS) kwa ajili ya sajili na Tanzania National Business Portal (TNBP) kwa ajili ya utoaji wa Leseni za Biashara Kundi A.
"Hatua hii inaenda kuboresha mazingira ya biashara nchini kwa kuwapunguzia gharama wafanyabiashara wetu kupitia kikao hiki, na Brelq itaonesha pamoja na mambo mengine taratibu za utoaji,"alisema.
Katibu mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Tawala za Mikoa (TAMISEMI) Aldof Ndunguru alisema mpango wa maendeleo ambao unatekelezwa Sasa dira yake ni kuifanya nchi kuwa shindani,na ili kuwa shindani ni kuhakikisha utekelezaji wa maeneo wezeshi, yakiwemo yanayozalishwa yanauzwa na yanakuwa na tija.
Akawataka maafisa Biashara hao kufanyakazi kwa ufasaha mchango mkubwa utatekelezeka na kufikia azma ya nchi ya uchumi shindani.
No comments:
Post a Comment