HATIMILIKI 71000 KUTOLEWA BARIADI NA MRADI WA LTIP - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Wednesday 15 May 2024

HATIMILIKI 71000 KUTOLEWA BARIADI NA MRADI WA LTIP

 




Na Mwandishi Wetu, Bariadi


maipacarusha20@gmail.com 


Vijiji takribani 41 katika Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi Mkoani Simiyu vitanufaika na Mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi (LTIP) kwa kutambuliwa, kupangwa, kupimwa na kumilikishwa ambapo takribani hatimiliki 71000 zitatolewa kwa wananchi.


Hayo yamebainishwa na Mkuu wa Wilaya ya Bariadi Bw. Simon Simalenga wakati wa kujadili utekelezaji wa Mradi huo katika ukumbi wa Bariadi, Leo tarehe 15 Mei 2024 Mkoani Simiyu.


Alisema zoezi la urasimishaji wa makazi ya wananchi litachochea matokeo chanya katika maendeleo ya Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi ikiwa ni pamoja na kuleta usalama wa milki za ardhi, kukukuza uchumi na kupunguza au kumaliza migogoro itokanayo na ardhi.


‘‘Kila kiongozi ajitahidi kusimamia eneo lake na kutoa ushirikiano kwa timu ya mradi ili lengo la kuwafikia na kuwahudumia watanzania litimie kwa kupatiwa hati miliki zitakazo wasaidia kujikwamua kiuchumi pindi watakapokuwa wanataka kukopa benki’’ alisema Simalenga.


Akimwakilisha Meneja Mradi kwa upande wa Mjini Bw. Paul Kitosi amesema kuwa michango ya sekta binafsi, Mashirika Yasiyo ya Kiserikali na Mashirika ya Kijamii katika kuendeleza na kutekeleza sera ya ardhi imetambuliwa na kuthaminiwa na Serikali yetu ya Jamhuri wa Muungano wa Tanzania kwa kupitia utekelezaji wa Mradi huu.  


‘‘Takribani asilimia themanini (80%) ya kazi zote za urasimishaji mijini zitatekelezwa na Makampuni binafsi yaliyosajiliwa kufanya kazi za upangaji (mipango miji) na upimaji wa ardhi aidha asilimia (20%) ya kazi hizo zinatekelezwa na Serikali kupitia watumishi walioko katika Halmashauri husika’’ alisema Kitosi.


Nae Bw. Martin Maige mwakilishi wa makundi maalum amesema kuwa wanamshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kwa kupeleka mradi huo na kuwapa kipaumbele watu wenye ulemavu hasa katika kupata elimu ya masuala ya ardhi.


Mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi (LTIP) unaotekelezwa na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi umeweka nguvu kubwa katika kutoa elimu kwa wananchi kuanzia ngazi ya Kitaifa, Wilaya, Mtaa/Kijiji mpaka Kitongoji ikiwa ni pamoja na kuzingatia haki za makundi mbalimbali wakiwemo wakulima, wafugaji, wavuvi, wanawake, Watoto, vijana, wenye ulemavu sambamba na utoaji wa elimu ya usawa wa jinsia katika umiliki wa Ardhi ili kuhakikisha usalama kwa kila mmili wa kipande cha ardhi kwa Mtanzania.

No comments: