RC MALIMA ATAKA VIKUNDI VYA WANAWAKE KUJIKITA KATIKA SHUGHULI ZA KIUCHUMI - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Wednesday 15 May 2024

RC MALIMA ATAKA VIKUNDI VYA WANAWAKE KUJIKITA KATIKA SHUGHULI ZA KIUCHUMI

 



MKUU wa Mkoa wa Morogoro Adam  Malima 




Na Lilian Kasenene, Morogoro 

maipacarusha20@gmail.com


MKUU wa Mkoa wa Morogoro Adam  Malima amevitaka vikundi vya wanawake Mkoani humo kujikita katika shughuli za kiuchumi hasa kilimo biashara kwa kuwa mazao mengi ya biashara na viungo yanaweza kulimwa katika maeneo mengi ya Mkoa huo.


Malima alisema hayo wakati akifunga kikao cha kutambulisha Program ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi inayojulikana kama Imarisha Uchumi na Mama Samia (IMASA), ambapo kikao hicho kilikuwa na lengo la kutoa elimu ya kuwajengea uwezo wafanyabiashara Wanawake Mkoani humo.


"Mnatakiwa mtengeze kikundi cha watu kumi au zaidi mpate mbegu za kokoa mpande hadi mvune, mkipata Mil. 20 au 30 mtachagua mgawane au muongeze biashara yenu hapo ni nyie wenyewe,"alisema mkuu huyo wa Mkoa.


Aidha Malima alisema shughuli za kiuchumi hasa Kilimo biashara kinaweza kufanyika katika maeneo mengi ya Mkoa huo ikiwemo Mvomero, Gairo (Nongwe) na Wilaya ya MorogoroDC (Mvuha) na kubainisha kuwa kilimo kimeongezewa thamani na Dk Samia Suluhu Hassani kwa zao la Kokoa kupanda bei kutoka shilingi 3,000 hadi 28,000 kwa kila kilo moja.


Katika hatua nyingine, Malima alisema kuwapa wananchi fedha  haimaanishi umewasaidia kwani uweshezaji wa kiuchumi ni muhimu kutoa pesa na elimu (maarifa) itakayowasaidia wananchi hususan wanawake kuongoza miradi yao na kuweza kufanya miradi yao kwa uhakika zaidi.


Kwa upande wake,Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi (NEEC) Being’i Issa alisema biashara ya uwezeshaji ni muhimu kufanya katika vikundi vilivyosajiliwa na Halmashauri na kutumia vikundi hivyo kuboresha biashara zao.


Sambamba na hilo, Katibu huyo alisema mwaka 2023/2024 kuna mipango mahususi ya kuhakikisha kunapatikana wananchi wengi zaidi wenye hali ya chini kuingia katika manunuzi ya uma, hivyo asilimia 30 itatakiwa kwenda kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.


Naye, Mwenyekiti wa Jukwaa la Uwekezaji kwa wakina mama wawekezaji Mkoa wa Morogoro Hadija Mbwana alisema wananchi hasa wanawake wamekuwa wakipoteza fursa nyingi kutokana na uhaba wa mitaji ambapo alisema benki zitaimarisha biashara zao kuleta tija kwao, jamii na Taifa kwa jumla.


Aliongeza kwa kuwashauri wanawake hao kuwa wanapaswa kujiunga kwenye vikundi mbalimbali kisha kuungana na kutengeneza viwanda vidogo vidogo ili kutengeneza ajira za kutosha hivyokujikwamua na umaskini.


No comments: