NCHI WANACHAMA WA MAKUBALIANO YA LUSAKA ZATAKIWA KUZIDISHA USHIRIKIANO KUZUIA UJANGILI NA BIASHARA HARAMU YA WANYAMAPORI NA MAZAO YA MISITU - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Sunday 30 June 2024

NCHI WANACHAMA WA MAKUBALIANO YA LUSAKA ZATAKIWA KUZIDISHA USHIRIKIANO KUZUIA UJANGILI NA BIASHARA HARAMU YA WANYAMAPORI NA MAZAO YA MISITU

 






Na. Anangisye Mwateba-Nairobi Kenya


maipacarusha20@gmail.com


Jitihada za pamoja katika kukabiliana na ujangili, biashara haramu ya usafirishaji wa wanyamapori hai na mazao yake; pamoja na mazao ya misitu ni chachu ya mafanikio katika utekelezaji wa Makubaliano ya Lusaka. Aidha, nchi wanachama zina wajibu wa kugharamia jitihada hizo bila kuchoka ili kulinda mafanikio yaliyopatikana.


Haya yamebainishwa na Rais wa Baraza la Uongozi la Mawaziri wa nchi wanachama wa Makubaliano ya Lusaka anayemaliza muda wake Mhe. Dkt. Alfred Mutua - Waziri wa Utalii na Wanyamapori wa Jamhuri ya Kenya alipokuwa akifungua Mkutano wa 13 wa Baraza hilo la Uongozi.


Vilevile katika hotuba yake Mhe. Mutua alitoa pongezi kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa uamuzi wake wa kujitolea kuteua na kumgharamia afisa kutoka Tanzania kuwa sehemu ya kikosi kazi kinachoratibu utekelezaji wa shughuli za kila siku za Makubaliano ya Lusaka yanayolenga kuwa na mikakati ya pamoja katika kupambana na wimbi la biashara haramu ya wanyamapori hai, nyara na mazao ya misitu.


Aidha, akiushukuru uongozi wa Baraza la Uongozi la Mawaziri kutoka nchi wanachama wa Makubaliano ya Lusaka, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Dunstan Kitandula(Mb) ambaye alimuwakilisha Mhe. Angella J. Kairuki (Mb) - Waziri wa Maliasili na Utalii alisema kuwa kikosi kazi kinachoratibu utekelezaji wa shughuli za kila siku za Makubaliano ya Mkataba wa Lusaka kimefanya kazi kubwa katika kuimarisha shughuli za uhifadhi kwa kubuni mbinu mpya za kupambana na ujangili wa wanyama pori na mazao ya misitu.

Mhe. Kitandula aliongeza kuwa ushirikiano uliopo kati ya nchi wanachama katika kupashana habari na jitihada za pamoja kupambana na ujangili na mienendo ya biashara haramu kumewezesha kudhibiti na kupunguza vitendo vya ujangili na biashara haramu; na hivyo kulinda na kuhifadhi maliasili za bara la Afrika.


Mhe. Kitandula alitumia nafasi hiyo kuzikakaribisha nchi wanachama wa Makubaliano ya Lusaka kushiriki kwenye mkutano wa 14 unaotarajiwa kufanyika nchini Tanzania mwaka 2025.



“Nashauri kikosi kazi kiendelee kutoa elimu kwa nchi nyingi zaidi ili zijiunge kwenye kutekeleza  makubaliano ya Lusaka na hivyo kulinda na kuhifadhi maliasili zilizopo katika bara la Afrika kwa vizazi vya sasa na vizazi vijavyo”. Alisema Kitandula. 


Mkataba wa Makubaliano ya Lusaka ambao utekelezaji wake ulianza miaka 13 iliyopita una lengo la kupambana na kuzuia biashara haramu ya usafirishaji wanyamapori hai na mazao yake pamoja na usafirishaji haramu wa mazao ya misitu.

No comments:

Post a Comment