JKIC KUTUMIA HOSPITALI YA WILAYA NAMTUMBO KAMA KITUO KIDOGO CHA UCHUNGUZI NA MATIBABU YA MOYO - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Wednesday 10 July 2024

JKIC KUTUMIA HOSPITALI YA WILAYA NAMTUMBO KAMA KITUO KIDOGO CHA UCHUNGUZI NA MATIBABU YA MOYO

 




Na Mwandishi wetu,Namtumbo 


maipacarusha20@gmail.com


Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete JKCI inatarajia kuitumia Hospitali  ya Wilaya Namtumbo kama kituo kidogo cha  uchunguzi na Matibabu ya moyo ili kusaidia wananchi wenye hali chini mkoani Ruvuma na mikoa jirani kupata matibabu.


Nia ya taasisi hiyo ya JKCI ni kuwapunguzia gharama wananchi wanayoishi na kusafiri umbali mrefu kwenda kupata matibabu.


Hayo yalielezwa na Mbunge wa jimbo la Namtumbo Vita Kawawa  wakati wa uzinduzi wa kambi ya maalumu ya uchunguzi  na matiabu ya moyo ambayo inaendeshwa na Madaktari bingwa tisa wa moyo  toka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete.


Kawawa alisema Mkurugenzi wa Taasisi ya JKCI Dk.Peter Kisenge ameahidi  kupeleka vifaa na wataalam ili kusaidia kutibu wananchi wenye matatizo ya moyo  pamoja na kuwapatia watumishi  mafunzo ya awali ya  kutumia vifaa  ili kutoa tiba ya awali ya utambuzi wa ugonjwa wa moyo.


Alisema,kupelekwa kwa huduma ya matibabu ya moyo  wilayani humo kutasaidia kupunguza kero ya wananchi kusafiri umbali mrefu kwenda kufata huduma ya matibabu Hospitali ya Rufaa Muhimbili , Bugando na KCMC.


"Namshukuru mkuu wa JKCI  kwa kutupatia  wataalam hawa, pia ameahidi kutuletea vifaa na kututafutia wafadhili na ametangaza kwanzia sasa Hospitali  ya Namtumbo itakuwa kituo kidogo cha JKCI ili wananchi waweze kupatiwa matibabu hapahapa na madaktari bingwa toka JKCI;"alisema Mbunge Kawawa


Aidha alimshukuru Rais Samia Suluhu kwa kuleta huduma  ya mkoba katika wilaya  hiyo kwani itatusaidia wananchi na pia ameweza kupeleka vifaa tiba, Dawa na hata kuboresha miundombinu ya majengo


Naye Kiongozi wa Madaktari  bingwa  tisa wa moyo Dk Baraka Ndelwa toka JKCI alisema , Wagonjwa wote watakaojitokeza watapatiwa matibabu hata kama ni usiku .


" Tunauzoefu wa wa kuhudumia wagonjwa wasiopungua 400 na watahakikisha wanawahudumia wagonjwa wote  ambao watajitokeza."alisema Dk Ndelwa.


Naye Dk Aaron Hyera ,alisema wataalam watawasaidia wananchi wenye uwezo mdogo kupata  uchunguzi wa afya zao na matibabu  wakiwa kwenye maeneo yao 


"Hii ni mara ya tatu kwa madaktari  bingwa kuweka kambi wilayani hapo hivyo amewataka wananchi wajitokeze kwa wingi ili kuweza kupata  matibabu."alisema Dk Hyera


Naye Theodora Mhuwa mkazi wa kijiji cha Likuyuseka alisema ameteseka kwa muda mrefu na ugonjwa wa moyo  kutokana na kutokuwa kuwa na uwezo wa kupata fedha za matibabu hivyo alishakata tamaa  na kusubiri kifo  hivyo kupelekwa kwa huduma hiyo kutasaidia wananchi kupata huduma za moyo toka kwa madaktari bingwa.


Kwa upande wake Halima Shauri  mkazi wa kijiji cha Njalamatata alisema amepitia mateso ya kusafiri  mara kwa mara kwenda Hospitali ya Taifa Muhimbili kutibiwa tatizo la moyo hivyo kupelekwa kwa huduma  hiyo kumerejesha matumaini mapya kwa wagonjwa wa moyo.


"Niwaombe wananchi wajitoleze  kufanyiwa uvhunguzi na kutibiwa ili waweze kufahamu matatizo yanayowakabili,"alisema.



No comments: