MAIPAC yazindua mradi wa Mazingira, kupewa kiwanja Monduli. - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Saturday 6 July 2024

MAIPAC yazindua mradi wa Mazingira, kupewa kiwanja Monduli.

 

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Monduli Isack Joseph akiwa na watu wa jamii ya wahadzabe na wadatoga mara baada ya uzinduzi wa mradi wa Uhifadhi wa mazingira kwa kutumia maarifa ya asili 


Mkurugenzi wa shirika la wanahabari la usaidizi wa jamii za pembezoni MAIPAC, Mussa Juma akiwa pamoja na watu wa jamii ya wahadzabe na wadatoga mara baada ya uzinduzi wa mradi.

Mkurugenzi wa Maipac, Mussa Juma akieleza mradi wa Uhifadhi wa mazingira kwa kutumia maarifa ya asili mbele ya wanufaika wa mradi huo jamii ya wahadzabe, wadatoga na wamasai.


Halima Mollel mkazi wa Selela akifurahia taarifa za Ujenzi wa uzio katika chanzo Cha maji Selela 



Mwandishi wetu, MAIPAC 


maipacarusha20@gmail.com 


Taasisi ya wanahabari ya usaidizi wa Jamii za Pembezoni (MAIPAC) imezindua mradi wa uhifadhi wa mazingira kwa kutumia maarifa ya asili huku Mwenyekiti wa Halmashauri ya Monduli ameahidi kutoa kiwanja kwa ajili ya ujenzi wa kituo Cha kujifunza maarifa ya asili.


Mradi huo wa Mazingira unafadhiliwa na Mfuko wa Mazingira Duniani(GEF) kupitia program ya miradi midogo ambayo inasimamiwa na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) na kuratibiwa na Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira).


Mwenyekiti wa Halmashauri ya Monduli mkoa wa Arusha, Isack Joseph amezindua mradi huo leo, Julai 6, 2024, katika hafla iliyofanyika hoteli ya Makambo te makuti iliyopo Kigongoni mto wa Mbu wilaya ya Monduli Mkoani Arusha.


Joseph akizungumza katika uzinduzi huo , aliipongeza taasisi ya wanahabari ya MAIPAC kwa kubuni mradi huo ambao unasaidia vita dhidi ya athari za mabadiliko ya Tabia nchi.


"Nawapongeza MAIPAC  kwa kuja na mradi huu kwanza  kujenga uzio katika chanzo cha maji cha Kabambe kata ya Selela lakini pia katika eneo la Eyasi kwenda kukusanya maarifa ya asili katika uhifadhi"alisema


Mwenyekiti huyo, alisema halmashauri hiyo ipo tayari kutoa ardhi kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha kuhifadhi maarifa ya asili ambapo watu watakuja kujifunza Mila ,Tamaduni na maisha ya jamii za asili.


"Nimesikia maombi ya Mkurugenzi wa MAIPAC, Mussa Juma kuomba ardhi kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha maarifa ya asili sisi tupo tayari kutoa ardhi tunaomba kuletewa barua rasmi ya maombi"alisema


Awali Mkurugenzi wa MAIPAC, Mussa Juma alisema mradi huo unatekelezwa kwa awamu ya pili awamu ya kwanza ilikuwa wilaya za Longido, Ngorongoro na Monduli na Sasa ni wilaya mbili za Karatu na Monduli .


Alisema lengo la mradi huo ni kusaidia uhifadhi wa mazingira, vyanzo vya maji na Misitu kwa faida ya sasa na vizazi vijavyo .


"Tumebaini Kuna maarifa mengi ya asili ya uhifadhi mazingira hivyo MAIPAC tunakwenda kuyakusanya katika nakala ngumu na laini na baadae kutengeneza kitabu kwa awamu ya pili "alisema


Juma alishukuru GEF,UNDP na Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira kuendelea kutoa fedha kwa MAIPAC ili itekeleze miradi ya mazingira na kutunza vyanzo vya maji.


Akizungumza Kituo Cha kutunza maarifa ya asili alisema wanaomba kupatiwa ardhi ili kuanza mikakati ya ujenzi wa kituo ambacho pia kitakuwa kitega uchumi kwa jamii za pembezoni.


Awali Afisa Misitu wilaya ya Karatu, Reginald Hallu alisema wilaya hiyo kama wilaya nyingine zinakabiliwa na changamoto ya uharibifu na mazingira hasa kwa wananchi kulima katika vyanzo vya maji.


Hallu alisema halmashauri imekuwa  ikichukuwa hatua mbalimbali Kudhibiti na akapongeza MAIPAC kuungana na serikali na kupeleka mradi wa mazingira lake Eyasi.


Naye Afisa misitu tarafa ya Manyara, Happy Masaki alisema mwaka juzi MAIPAC ilikuwa na mradi wa mazingira katika kata ya Selela na aliomba wajengewe uzio katika chanzo Cha maji Kabambe na anashukuru MAIPAC kukubali na mwaka huu wanajenga.


Wakizungumza katika uzinduzi huo wananchi wa Selela na Eyasi walipongeza MAIPAC kuja na mradi huo na kuahidi wataendelea kutoa ushirikiano.


Halima Mollel mkazi wa Selela alisema wanaipongeza Taasisi ya wanahabari ya MAIPAC kurudi katika kata ya Selala kutekeleza mradi wa ujenzi wa uzio katika  chanzo cha maji Kabambe..


Afisa miradi wa Shirika la Jumuiko la Maliasili Tanzania (TNRF) Stevin Ngowi na Mkurugenzi wa Shirika la MPDO ,Lebaraka Laizer ambao mashirika Yao yanafadhiliwa na UNDP pia walieleza MAIPAC limekuwa Shirika la mfano kwa kutekeleza vyema miradi.


Ngowi aliomba halmashauri ya Karatu na wananchi wa Eyasi kushirikiana vizuri na MAIPAC kama ilivyokuwa wilaya za Longido , Ngorongoro na Monduli .


No comments: