Maisha ya Wahadzabe hatarini wavamiwa Makazi Yao. - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Thursday 11 July 2024

Maisha ya Wahadzabe hatarini wavamiwa Makazi Yao.

 






Na: Mussa Juma, maipac 


maipacarusha20@gmail.com


Jamii ya Wahadzabe( Indigenous community) inayoishi  wilayani Karatu, mkoa Arusha, maisha yao yapo hatarini, baada ya maeneo wanayoishi kuvamiwa na makundi ya wakulima na wafugaji na hivyo, kuanza kukosa chakula na mahitaji mengine.


Jamii hii  maisha yao, hutegemea kula wanyapori, mizizi, matunda na asali kwa sasa imebaki na watu takriban 500 tu  katika wilaya hiyo.


Wakizungumza na waandishi wa habari, waliofika katika maeneo yao, kupata maarifa yao ya asili katika uhifadhi ya mazingira, kupitia mradi unaotekelezwa na Taasisi ya wanahabari ya kusaidia jamii za pembezoni(MAIPAC) kwa ufadhili wa Mfuko wa Mazingira Duniani(GEF) kupitia program ya miradi midogo ya Shirika la Maendeleo la umoja wa mataifa (UNDP) na Ofisi ya Makamu wa Rais- Mazingira, jamii hiyo iliomba msaada wa haraka.


Kiongozi wa jamii hiyo, katika kambi ya Murusi kijiji cha Qang’dend kata ya Baray, Karatu, Ng’washambi Kusombi alisema wao, kwa kutumia maarifa yao ya asili waliweza kutunza mazingira, misitu na vyanzo vya maji, lakini sasa wapo hatarini kukosa chakula na mahitaji mengine.


Kusombi alisema jamii za wakulima na wafugaji, wamevamia maeneo yao, kuanza kulima na kufuga na wengine kukata miti na kuchoma mkaa hali ambayo imeanza kuwasabisha adha kubwa na kutishia maisha yao.


“zamani tulikuwa tunapata wanyamapori maeneo ya karibu tu, sasa tunatembea umbali mrefu sana, tulikuwa tunapata matunda na mizizi lakini sasa imepungua kwani miti inakatwa na wachoma mikaa”alisema


Alisema hata asali ambayo ndio hutegemea kwa chakula cha kila siku sasa imeanza kupotea kwani miti imekatwa na baadhi iliyopo imeanza kumilikiwa na jamii za wafugaji na wakulima waliowavamia.


“Tulikuwa tumeweka maeneo ya kupata asali katika miti haya mibuyu lakini sasa tukitaka kupanda kutoa asali tunaambiwa sio yetu tena,ama tunalazimishwa kugawana asali na wanaodai eti miti ni yao”alisema


Alisema kuna baadhi ya viongozi wa vijiji ndio wamekuwa wakiuza ardhi yao kinyemela licha ya halmashauri ya wilaya hiyo, kuwaeleza ni mali yao ingawa hawajawapa hatimiliki.


Nyambulu Njegela  alisema hata wanyama wamekimbia mbali Zaidi kwani katika maeneo yao waliokuwa wamehifadhi mazingira, miti imekatwa.


“Hivi sasa tunasafiri umbali mrefu kufuata Wanyama  na sisi kwa kawaida tunawinda mnyama mmoja tu mkubwa wa kula na hatuwindi mpaka nyama yote iishi sasa hatupati wanyama kwa karibu”alisema


Alisema kama hali ya sasa isipodhibitiwa maisha yao yatakuwa hatarini kwa sababu hata katika mapango ya mawe ambayo walikuwa wakiishi, tayari pia yamevamiwa na jamii nyingine.


Juliana Yohana alisema adha kubwa kwa sasa wanayopata wanawake wahadzabe wanalazimika kutembea kwa miguu umbali mrefu kufuata maji na  mizizi ya chakula na dawa.


“Tunaomba mtusaidie ardhi yetu isivamiwe zaidi maana tunapata shida  sana sisi , unaona tuna watoto wadogo, wanakaa hata siku nzima bila kupata maji, shule hakuna na zahanati zipo mbali sana”alisema.


Andrea Ngobole Meneja miradi wa MAIPAC, alisema kupitia mradi huo wa kukusanya maarifa ya asili ambayo baadae wataandaa kitabu Cha maarifa hayo, wamebaini jamii ya Kihadzabe ipo hatarini kutoweka ni muhimu serikali kuingilia kati.


“Hii jamii imeifadhi mazingira haikati miti, hawalimi wala kuchoma mikaa sasa kuna wavamizi wengi ambao wanalima katika ardhi yao, wanakata mikaa na wamepewa ardhi na viongozi wa vijiji”alisema


Alisema kupitia mradi huo wa GEF/UNDP wanatarajia kusambaza maarifa hayo katika vyombo vya habari ili kusaidia Jamii kutunza mazingira, misitu na vyanzo vya maji


Kauli ya Halmashauri ya Karatu.


Akizungumza na waandishi wa habari, Mkuu wa Kitengo cha Maliasili na Uhifadhi wa Mazingira katika halmashauri ya Karatu, Donata Kimaro, alisema halmashauri hiyo imeanza kufuatilia uvamizi wa maeneo ya Wahadzabe.


Kimaro alisema tayari halmashauri hiyo, ilikwishaandaa mpango wa matumizi bora ya ardhi katika maeneo ya jamii hizo lakini, imebainika kuna changamoto bado ya uelewa kwa  baadhi ya  viongozi  wa vijiji na wananchi.


Afisa Misitu wilaya ya Karatu, Reginald Hallu alisema tayari halmashauri hiyo, imeanza kukamata watu wanaovamia ardhi na kujenga, kulima na kukata mikaa kinyume cha sheria.


“Tayari tunakesi kadhaa watu waliovamia maeneo ya Wahadzabe na kuanza kuchoma mikaa na baadhi wamelipa faini na kuondoka, hivyo tunatoa onyo ni marufuku kuvamia ardhi iliyotengwa kwa jamii ya wahadzabe”alisema.


MWISHO.

No comments: