MWENGE WAINGIA MANYARA KUTEMBELEA MIRADI 57 YA SHILINGI BILIONI 149 - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Friday 12 July 2024

MWENGE WAINGIA MANYARA KUTEMBELEA MIRADI 57 YA SHILINGI BILIONI 149

 

 





Na Mwandishi wetu, Hanang'


maipacarusha20@gmail.com 


MWENGE wa uhuru umeanza mbio zake Mkoani Manyara, ambapo utatembelea, kukagua, kuzindua na kuweka jiwe la msingi kwenye miradi 57 ya maendeleo ya thamani ya Sh149.5 bilioni.


Mkuu wa mkoa wa Manyara, Queen Sendiga akipokea mwenge wa uhuru kutoka kwa mkuu wa mkoa wa Singida, Halima Dendegu, katika shule ya sekondari Mwahu kijiji cha Gehandu, wilayani Hanang' amesema utakimbizwa kilomita 980.5 kwenye halmashauri saba.


Sendiga amesema mwenge huo utaweka jiwe la msingi miradi 17 ya thamani ya shilingi milioni 134, kuzindua miradi nane ya thamani ya shilingi 3.4, kufungua miradi minne ya thamani ya shilingi bilioni 1.3, kukagua na kuona miradi 28 ya shilingi bilioni 10.7.


Amesema mchanganuo wa fedha hizo ni nguvu za wananchi shilingi milioni 102.5, serikali kuu shilingi bilioni 72.8, halmashauri za wilaya shilingi milioni 169.7 na wadau wengine shilingi bilioni 76.5.


Ametaja halmashauri za wilaya ambazo mwenge huo utapita ni Hanang', halmashauri ya wilaya Mbulu, Mbulu mjini, halmashauri ya wilaya ya Babati, Babati mjini, Kiteto na Simanjiro.


"Nitumie fursa hiyo kuwashukuru sana wananchi wa Manyara kwa kuibua, kuanzisha, kuchangia na kuitekeleza miradi hii na kipekee ninawashukuru wadau wa maendeleo ambao wamechangia shughuli za maendeleo," amesema.


Kiongozi wa mbio za mwenye wa uhuru kitaifa mwaka 2024 Godfrey Mnzava amewapongeza wananchi wa Manyara kwa namna walivyoutendea vyema kwa namna walivyoupokea.


Mnzava amesema pamoja na jumbe nyingine mwenge wa uhuru kwa mwaka 2024 una ujumbe mahususi wa tunza mazingira na shiriki uchaguzi wa serikali za mitaa kwa ujenzi wa Taifa endelevu.


Mkuu wa wilaya ya Hanang' Alhamishi Hazali amesema ukiwa eneo hilo utatembelea, kuweka jiwe la msingi, kukagua na kuzindua miradi tisa ya thamani ya shilingi bilioni 12.4.


Meneja wa wakala wa maji na usafi wa mazingira vijijini (RUWASA) wilayani Hanang' Hurbert Kijazi amesema mradi wa maji wa Mogitu Gehandu uliowekwa jiwe la msingi na mwenge una thamani ya zaidi ya Sh8 bilioni.


Mkazi wa kata ya Gehandu, Yohana Wilson ambaye ameshiriki mapokezi ya mwenge huo amesema watanzania wanapaswa kuuenzi kwani unatoa ujumbe wa kitaifa na kupitia miradi ya maendeleo.


"Kupitia mwenge tunaona miradi mbalimbali ya maendeleo ikiinufaisha jamii kiwemo ya sekta ya maji, elimu, afya na mingineyo," amesema.


No comments: