RC MALIMA ATOA MAAGIZO KWA MKURUGENZI WA MANISPAA MOROGORO JUU YA BABA NA MAMA LISHE WA SGR MOROGORO - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Sunday 14 July 2024

RC MALIMA ATOA MAAGIZO KWA MKURUGENZI WA MANISPAA MOROGORO JUU YA BABA NA MAMA LISHE WA SGR MOROGORO

 





Na: Lilian Kasenene, Morogoro 


maipacarusha20@gmail.com


MKUU wa mkoa wa Morogoro Adam Malima amempa wiki mbili Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro Emanuel Mkongo kutenga eneo na kujenga vibanda kwa ajili ya mama na baba lishe wanaotoa huduma nje ya stesheni ya SGR ili waweze kufanya biashara katika mazingira safi, salama na yenye hadhi.


Malima alifikia uamuzi wa kutoa muda huo baada ya kufanya ziara katika stesheni hiyo na kukuta mama na baba lishe wakipanga vyakula chini huku wateja wao wakiwemo abiria wanaosubiri treni wakila chakula wakiwa wamesimama.


Mkuu huyo wa mkoa alisema kuwa stesheni hiyo ni ya kisasa hivyo huduma zote zinazotolewa katika stesheni lazima ziwe za kisasa badala ya ilivyosasa ambapo mama na baba lishe wamekuwa wakiuza vyakula kwenye eneo lisilokuwa rasmi na pia lisilokuwa na ubora.


"Hii ni treni ya kisasa, hapa wanakuja abiria kutoka maeneo mbalimbali na hata wakigeni Mkurugenzi hakikisha ndani ya ndani ya wiki mbili hawa kina mama lishe na baba lishe wanatengenezewa mazingira bora ya kufanyia biashara zao nje ya stesheni hii, najua hilli halikushindi kwa sababu hujengi ghorofa unatakiwa kujenga mabanda yenye ubora," alisema Malima.


Awali mama na baba lishe hao wamemuomba mkuu wa mkoa kuona namna atakavyowasaidia katika kukuza mitaji yao ambapo mkuu huyo wa mkoa amemtaka Afisa maendeleo ya manispaa ya Morogoro kukutana na mama na baba lishe hao kwa ajili ya kuwaelekeza namna ya kuunda vikundi vitakavyowafanya wapate mikopo.


Mmoja wa akina mama wanaouza Matunda Telesia Daud aliuomba uongozi wa SGR kuwatengea maeneo wafanyabiashara wa matunda nje ya stesheni hiyo.


Kwa upande wa madereva wa bodaboda na bajaji Malima aliwataka madereva hao kuwa waaminifu kwa abiria wanaowabeba ambapo pia amewatoa hofu kuwa Serikali ipo pamoja nao katika kuhakikisha wanatoa huduna bora na za kisasa.


Pia Malima aliwataka madereva hao wa bajaji na bodaboda kuwa nadhifu wakati wote na kuvaa vikoti vyenye namba na jina la kituo hicho cha SGR wanachoegesha.


Akieleza changamoto zinazowakabili katika utendaji kazi wao mmoja wa madereva wa bodaboda Emanuel Jacob amesema kuwa ni pamoja kukosekana kwa choo nje ya stesheni hiyo ambacho wangeweza kukitumi badala ya ilivyosasa ambapo wanalazimika kuingia ndani ya stesheni ama kujisaidia haja ndogo vichakani.


Jacob ametaja changamoto nyingine kuwa ni kukosekana kwa huduma ya maji ya bomba kwa ajili ya kunywa hivyo ameuomba uongozi wa SGR kupitia kwa mkuu huyo wa mkoa kuwawekea tenki la maji.


Naye Athuman Hamisi mjumbe wa chama cha wasafirishaji abiria kwa bajaji na bodaboda kijiwe cha stesheni ya SGR alisema kijiwe hicho kina jumla ya bajaji zaidi ya 1000, bodaboda 250 na taksi 50 ambapo wote wanatoa huduma ya kubeba abiria kutoka kwenye stesheni hiyo na kuwapeleka maeneo mengine ya mji wa Morogoro.


Amesema jana Julai 11 madereva wa bodaboda wamefanya uchaguzi na kupata viongozi wao hivyo amemtoa wasiwasi mkuu huyo wa mkoa kuwa abiria wanaopanda vyombo hivyo wako salama.


Akitoa taarifa ya utendaji kazi wa stesheni hiyo mkuu wa kitengo cha habari na mawasiliano kutoka Shirika la reli nchini TRC Jamila Mbaruk amesema hali ya usalama katika stesheni hiyo ni asilimia 100 kwa kuwa zimefungwa kamera (CCTV camera) kwa ajili ya kuangalia abiria tangu anapoingia stesheni hadi anapopanda treni.


Aidha kamera hizo zimefungwa ndani ya treni kwa ajili ya kuangalia usama wakati wote wa safari na pia wapo askari ambao wamekuwa wakipita kuona hali ya usalama wa abiria.


Mwisho.

No comments: