Na Lilian Kasenene,Morogoro
maipacarusha20@gmail.com
MKUU wa mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila amesema mpango mkakati umeandaliwa na kuwasilishwa Wizara ya Kilimo na kupitia wadau kuweza kupata fedha za kuuboresha zaidi viwanja vya maonesho wa Nane Nane wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere , Kanda ya Mashariki ili uwe na hadhi ya kifaifa na kimataifa.
Chalamila alisema hayo mjini Morogoro wakati wa kikao cha maandalizi ya Nane Nane ya Kanda ya Mashariki yanayofanyika Viwanja vya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na kujumuisha halmashauri za mikoa ya Tanga, Pwani , Dar es Salaam na Morogoro.
“Mtakumbuka kwa miaka mingi tumekuwa na uwanja ambao bado haina hadhi kubwa , lakini sasa kuna andiko ambalo linaandaliwa na ambalo litapelekwa wizara ya Kilimo , tunaamini pia kupitia wadau , uwanja wetu unaweza kupata fedha za kuuboresha zaidi “alisema Chalamila.
Mkuu huyo wa mkoa alitaja baadhi ya maeneo ya maboresho ni kwenye mwonekano wa majengo, miundombinu ya barabara na maji , kuwa na maeneo ya mapumzuko , maeneo ya kuvutia michezo mbalimbali ya watoto na watu wengineo .
Pia alisema kilimo kinapaswa kuwa na mlengo mkubwa wa kuwasaidia wakulima na wafugaji, hivyo ni wajibu kuyaboresha maonesho ya Nane Nane kwa kuhamasisha zaidi, kuwa na wadau mbalimbali ambao wanaweza kuhudhuria kuonesha na wanaoweza kuhudhuria kununua bidhaa zao.
Chalamila alisema ni muhimu zaidi kuona namna ya kumkutanisha wakulima , wafugaji na masoko pale wanapoleta bidha zao badala ya kuamini ya kwamba wanakuja kuionesha.
“ Sisi tunafurahia kuziona kwani kikubwa wanaleta bidhaa zao ili kuiona , kuzipenda na kuweza kuzinunua” alisema Chalamila.
Mkuu wa mkoa huyo alitumia fursa hiyo kuwahamasisha wananchi wote kuwa waamshwe na kengere ya Nane Nane , kwani Nane Nane yam waka huu (2024) ni ya kipekee kutokana na kuwepo kwa mvua nyingi lakini hazijaathiri upatikanaji wa mazao.
“ Ni baadhi ya maeneo machache yameathirika kidogo hasa kwenye mazao ya mpunga ambacho kinatengemea kiwango fulani cha maji mashambani lakini kwa asilimia kubwa mazao yamepatikana “aliisema
Mkuu wa mkoa aliwataka wananchi kujitokeza kwa wingi kwenye viwanja hivyo kuona vipando , kuona mazao , mifugo na kuona teknolojia mbalimbali za kilimo, mifugo na uvuvi hasa ikizingatiwa katika zama hizi ni kilimo kinacholenga zaidi udhibiti kasi ya mabadiliko ya tabianchi.
Kwa upande wake Katibu Tawala wa mkoa wa Morogoro, Dk Mussa Ali Mussa alisema Sh milioni 50 zimetolewa kwenda mamkala ya usimamizi wa huduma ya maji ili kuchimba visima viwili kwa ajili ya matumizi ya umwagiliaji vipando na mengine .
No comments:
Post a Comment