Wanachama THRDC walaani utekaji watoto,wataka adhabu Kali. - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Sunday 28 July 2024

Wanachama THRDC walaani utekaji watoto,wataka adhabu Kali.

 




Mwandishi wetu, maipac.


maipacarusha20@gmail.com



Wanachama wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC ) Kanda ya Ziwa, wametoa  tamko la kulaani wimbi na utekaji watoto na kutoa mapendekezo ya kukabiliana na matukio hayo.


Katika tamko la pamoja la wanachama wa THRDC lililojumuisha  wanachama wa Mikoa ya Mwanza, Mara, Simiyu, Shinyanga, Geita na Kagera wameitaka serikali na jamii kuchukuwa hatua za kukomesha matukio ya ukiukwaji wa Haki za binaadamu kwa watoto. 


Katika tamko hilo lililosainiwa na Mratibu kanda ya ziwa Mashariki Sophia Donald, na Kanda ya Ziwa Magharibi chini ya mratibu Madaga Joseph wametaka hatua za haraka kuchukuliwa kukomesha matukio ya ukiukwaji wa Haki za Binaadamu.


Wameeleza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan wakati anaongea na viongozi wa kimila akizungumza kukemea matukio haya na sisi tunasisitiza viongozi wawajibike kwa kutimiza majukumu yao hasa wale wanaosimamia taasisi za ulinzi na usalma wa raia. 


"Sisi watetezi wa haki za binadamu tunaamini kwamba maelekezo ya  Rais si tu kwa viongozi wa serikali bali hata kwa viongozi wengine wa jamii kama viongozi wa dini pamoja na viongozi wa Mashirika yasiyo ya kutetea haki za binadamu. Hivyo, kutokana na msingi huo, sisi  katika mkutano wetu mkuu wa kanda tumeweka mikakati  kuhusu kukabiliana na changamoto hii pamoja kuamua  kutoa tamko hili kuhusu hali ya matukio ya utekwaji wa  watu na watoto katika kanda ya ziwa" wameeleza wanachama hao.


Watoa Takwimu za ukubwa wa tatizo 


Kwa mujibu wa takwimu za Jeshi la Polisi mwaka 2023 jumla ya watoto 73 walitekwa ama kuibiwa na kati yao, watoto 33 walitekwa kutoka kanda ya ya ziwa. Lakini pia kwa kipindi cha mwaka 2005 hadi 2024 jumla ya matukio ya watu 20 ya mauaji au utekwaji wa watu wenye ualbino yamesharipotiwa kanda ya ziwa ambapo kwa mwaka wa 2024 ni matukio 3 yameshatokea na kuripotiwa kwenye vyombo mbalimbali vya habari nchini. 


Wameeleza Mei 04, 2024 mtoto mwenye ualbino aitwaye Kazungu Julius mwenye umri wa miaka kumi (10) mkazi wa katoro mkoani Geita alinusurika kifo majira ya saa mbili usiku baada ya kuvamiwa na watu wasiyojulikana na kumkata mapanga sehemu mbalimbali za mwili wake hali iliyopelekea kuvuja damu nyingi.


Mnamo Mei 30, 2024 liliripotiwa tukio la kutekwa kwa mtoto wa miaka miwili (2) mwenye ualbino aitwaye Asimwe Novati lililofanywa na watu ambao hawakutambulika wakati huo katika Kijiji cha Bulamula, Kitongoji cha Mbale, Kata na Tarafa ya Kamachumu wilayani Muleba mkoani Kagera. Iliripotiwa kuwa watu hao walimvamia kwa kumkaba mama wa mtoto huyo Kebyera Richard, na kisha kumchukua na kukimbia na mtoto huyo kusikojulikana. Siku ya tarehe 17 Juni, 2024 iliripotiwa kupatikana kwa mwili wa mtoto huyo ukiwa umekatwa viungo vyake ikiwemo mikono, ulimi na macho. 


Baada ya kupatikana mwili wa mtoto huyo, tarehe 18 Juni, 2024 Mhe. Samia Suluhu Hassan katika Kongamano la Maendeleo ya Sekta ya Habari, alieleza masikitiko yake na kuumizwa sana na tukio la mauaji ya mtoto Asimwe Novati. Tunafahamu kwamba kuna watu tayari wameshakamatwa na kufikishwa mahakamani kuhusu tukio hili na tuna imani na Mahakama kuwa itatenda haki katika jambo hili. 


Joseph  amefafanua 3 Novemba 2022, Mathias Dida Songoma alikatwa mkono wa kulia na kupelekea kifo chake katika kijiji cha Ngula wilayani Kwimba mkoani Mwanza. 


Wamesema Disemba31 2023 Happiness Raphael mwanafunzi wa chuo cha Mtakatifu Agustino (SAUT) Mkoani Mwanza aliyekuwa anasoma mwaka wa kwanza alishambuliwa kwa kujeruhiwa na panga na watu wasiojulikana muda wa saa 3 usiku katika eneo la Malimbe katika chuo SAUT. 


Tarehe 25 Juni 2022 Iyani Donald alivamiwa na kundi la watu wasiojulikana wakati wakiwa wamelala usiku na kunusurika kifo baada ya kufanikiwa kujinasua wilayani Sengerema mkoani Mwanza. 


"Matukio ya kutekwa na kupotezwa  kwa watu wazima na  watoto hayatokei kanda ya ziwa tu bali yanatokea nchi nzima kwa mfano tarahe 23 ulai 2024 watoto wawili walinusurika kutekwa Tabata Kisiwani jijini Dar es Salaam ambapo mtekaji alikamatwa na ndio ilikuwa ponapona ya hao watoto. Jeshi la Polisi lilifanikiwa kumkamata mtuhumiwa huyo ingawa bado hajafikishwa Mahakamani kwa hatua za kisheria"wameeleza 


Katika hatua ya kushangaza Jeshi la Polisi mkoani Arusha limethibitisha jana Julai 25 kwamba watoto wawili wa familia moja Mordekai Maiko (7) anayesoma darasa la tatu na Masiai Maiko (9) anayesoma darasa la tano shule ya Msingi Olosiva, Arumeru Arusha, wamepotea katika mazingira ya kutatanisha baada ya kuaga kuwa wanaenda shule Julai 24, 2024 lakini hawakurudi nyumbani na hawajaonekana popote. Kamanda wa Polisi mkoa wa Arusha amekiri taarifa hiyo na kuahidi kulifanyia kazi tukio hilo. 


"Sisi tunaamini kwamba ukatili dhidi ya watu wenye ualibino unaweka taswira mbaya kwa nchi yetu na kuonyesha kuwa hakuna usalama kwa watu hususani watu wenye ualbino, tukio la kuuawa kwa mtoto Asimwe Novati ni tukio la kinyama, linalotweza utu wa mwanadamu na kurudisha upya taswira mbaya iliyotokea miaka michache dhidi ya ukatili wa watu wenye ualbino."lilisomeka tamko hilo.


Wameeleza mashambulizi dhidi ya watu wenye ualbino yamerudi kwa kasi katika kipindi hiki kuelekea uchaguzi hasa kwa watoto, itakumbukwa mwaka 2015 mkoani Rukwa lilitokea tukio la kushambuliwa kwa mtoto wa kiume aitwaye Baraka Cosmas mwenye umri wa miaka sita (6) akiwa amelala na mama yake mzazi ambapo watu wasiojulikana walivamia nyumbani kwao na kumkata kiganja. 


Sophia anasema matukio haya ya kinyama na kikatili dhidi ya watoto wenye ualbino yanapaswa kuikumbusha Serikali na mamlaka zote husika kuhusu  kukabiliana na unyanyasaji na ukatili dhidi ya watoto pamoja na watu wenye ualbino katika jamii zetu.


Matukio ya mauaji kwa watu wenye ualbino ni ukiukwaji wa haki ya kuishi iliyopo katika Ibara ya 14 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977, Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Watu wenye Ulemavu wa Mwaka 2006, Tamko la Ulimwengu Juu ya Haki za Binadamu la Mwaka 1948, Mkataba wa Afrika Juu ya Haki za Binadamu na Watu wa Mwaka 1981 pamoja na Kanuni ya Adhabu Sura ya 16. 


Pamoja na wimbi la kutekwa au kupotezwa kwa watoto, swala la watu wazima kupotezwa na kutekwa pia limekuwa likijitokeza katika kanda hii lakini wahusika bado hawajajulikana ni nani. Changamoto ni kuwa matukio haya hayaonekani kufanyiwa kazi au kufanyiwa uchunguzi wa kina na hivyo kupelekea matukio kuirudia kama inavyoonekana katika Taarifa ya Hali ya Haki za Watetezi na Nafasi za Kiraia Nchini ya mwaka 2023. 



       Watoa mapendekezo Tisa 


Tunalitaka Jeshi la Polisi la Tanzania ambalo ndio lenye dhamana ya kulinda usalama wa raia na mali zetu kuwajibika na linapaswa kuwa linachukua hatua za kuzuia matukio ya utekwaji ama mauaji kwa watu na  watoto nchini. Pia Jeshi la Polisi linapaswa kuwa linachukua hatua mapema na kutoa taarifa kwa umma haraka endapo kuna tukio lolote la kutekwa kwa watu,  watoto au watu wenye ualbino. Hatua za haraka zisipochukuliwa huongeza hofu kwa jamii  na hasa kwa watoto na  watu wenye ualbino kuhusu usalama wao nchini. 


Tunaiomba Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira, Vijana na Watu wenye Ulemavu) kumaliza haraka mchakato wa upitishwaji Rasimu ya Mpango Kazi wa Taifa kwa watu wenye Ualbino 2023/2024 - 2027/2028 ili hatua za utekelezaji ziweze kuchukuliwa.  


Tunaiomba Serikali hasa katika kipindi hiki cha kuelekeza uchaguzi wa Serikali za Mitaa na Uchaguzi Mkuu mwaka 2024/2025 kutenga bajeti maalumu ili kuimarisha mifumo ya ulinzi wa watoto na kwa watu wenye ualbino, hii ni katika ngazi zote kuanzia Kitongoji, Kijiji, Kata, Wilaya, Mkoa na Kifaifa ili kuhakikisha maisha ya watu wenye ualbino yanalindwa na watu hao waendelee kufurahia maisha yao kama watu wengine katika jamii.


Tunatoa wito kwa jamii kuripoti watu wote wanaojihusisha na vitendo vya utekaji wa watoto na mauaji kwa watoto wenye ualbino ili vyombo vya ulinzi na usalama ziweze kuwachukulia hatua za kisheria. 

 

   Tunatoa wito kwa jamii pia kuachana na imani potofu juu ya matumizi ya viungo vya watu wenye ualbino kwa kuhusisha na utajiri au kujipatia mamlaka katika ngazi mbalimbali.Tunawahimiza wanajamii wote kusimama pamoja kuibua na kutoa taarifa juu ya watu wote wanaofanya vitendo vya kikatili dhidi ya watu wenye ualbino kwa sababu ya imani za kishirikina. Sambamba na hili tunatoa wito kwa Mashirika na serikali kuendelea kutoa elimu dhidi ya imani za kishirikina zinazosababisha mauaji ya watu wenye ualbino.


Tunapenda kuikumbusha Serikali kuwa, mapema mwaka huu wa 2024, Kamati ya Umoja wa Mataifa ya Haki za Watu Wenye Ulemavu (CRPD) ilieleza masikitiko yake kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuhusu ufuatiliwaji hafifu kuhusu matukio ya ukatwaji viungo vya watu wenye ualbino na Serikali kutowajibika dhidi ya matukio hayo, Kamati hiyo ilisema kwamba, kushindwa kwa Tanzania kulaani na kuchunguza mashambulizi dhidi ya watu wenye ualbino ni ukiukwaji mkubwa wa wajibu wake wa kuwalinda watu wenye ulemavu nchini.


Tunatoa wito kwa Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuunda Tume Huru kwaajili ya kuchunguza matukio ya utekwaji wa watu nchini na Tume hiyo pia ichunguze tuhuma za matukio ya utekwaji wa watu yaliyoripotiwa kuwa vyombo vya dola vinahusika katika matukio hayo. Malalamiko haya yamekuwepo kwa miaka mingi lakini hakuna chombo huru cha kushughulikia masuala haya ambayo yanachafua taswira ya nchi.


Tunatoa wito kwa Serikali kuridhia mkataba unaozuia masuala ya utesaji wa watu (Convention Against Torture) pamoja na Mkataba wa Usalama wa Watu dhidi ya Utekaji na Upotezwaji wa Watu. 


 Viongozi wote nchini wa serikali, wa vyama , wa tasisi za kidini na asasi za kiraia wajitokeze kukemea matukio haya na wale wenye dhamana ya kulinda usalama wa raia wachukue hatua kama  Rais alivyohimiza.  


Mwisho

No comments: