WATU 12 WADAIWA KUUGUA KIPINDUPINDU MANISPAA MOROGORO,ELIMU YATAKIWA KUTOLEWA - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Wednesday 17 July 2024

WATU 12 WADAIWA KUUGUA KIPINDUPINDU MANISPAA MOROGORO,ELIMU YATAKIWA KUTOLEWA

 


Na Lilian Kasenene,Morogoro


maipacarusha20@gmail.com


UGONJWA wa Kipindupindu unadaiwa kuibuka kwenye kata za Lukobe, eneo la Yespa kata ya Kihonda, kichangani, Mazimbu na eneo la kasanga Mindu katika Manispaa ya Morogoro ambapo zaidi ya wagonjwa 12 wamefikishwa na kulazwa katika kituo cha afya cha Sabasaba wakikabiliwa na changamoto ya ugonjwa huo na wanapatiwa matibabu.


Wagonjwa hao waliofikishwa kituoni hapo walikutwa na waandishi wa habari waliofika kituoni na mmoja wa waandishi wa habari aliyejifanya mgonjwa na kwenda kupata matibabu, ambapo walikuwa wamelazwa sakafuni, kwenye benchi ya kukaa wagonjwa, vitanda pamoja na karo la kunawia mikono.


Akizungumza na Waandishi wa Habari hao mganga wa zamu katika kituo cha afya Sabasaba Dk Facilius Zanzibar alisema yeye aliingia zamu saa nane mchana na kutakiwa kutoka saa mbili usiku lakini mpaka saa tano usiku waandishi wanafika kituoni hapo aliendelea na kazi kutokana na uwepo wa wagonjwa wengi wa kuhara na kutapika wakidaiwa kuwa ugonjwa wa kipindupindu.


Dk Zanzibar alisema kituo hicho cha Sabasaba limekuwa kikipokea wagonjwa wa kuharisha maji meupe na kutapika mfululizo ambapo dalili hizo zote ni za kuugua ugonjwa wa Kipindupindu.


Licha ya Waandishi wa Habari kupata maelezo kutoka kwa Dk Zanzibar, Idara ya afya katika Manispaa ya Morogoro ilipoulizwa ili kuzungumzia uwepo ugonjwa huo iligoma.


Timu ya Waandishi wa habari ilifika ofisi ya mganga mkuu Manispaa ya Morogoro Dk Focus Maneno ili azungumzie mlipuko huo wa magonjwa ya kuhara na kutapika ama kipindupindu kama alivyoahidi siku moja kabla, baada ya kukutana naye(usikuwa kuamkia julai 16) katika  kituo cha afya cha sabasaba aligoma kuzungumza.


Dk Maneno alidai awezi kuzungumza hadi timu ya wataalamu wake imalize kufanya tathmini ya hali hiyo na kwamba sio kila anayeharisha na kutapika ni mgonjwa wa kipindupindu.


Aidha Dk Maneno aliwataka wanahabari kumtafuta afisa habari wa manispaa hiyo ili ampe mganga huyo mwongozo wa kuzungumzia tukio hilo, na licha ya afisa habari huyo kutafutwa na kuelezwa hali mbaya iliyokutwa kituo cha afya cha sabasaba, kwa wagonjwa  12 wa kuhara na kutapika kukutwa wamejaa hospitalini hapo na kukosa vitanda, na kulazimika kulala chini, kwenye mabenchi, chumba cha datari na kwenye masinki ya maji,ambaye alisema mganga huyo alisema hadi amalize kufanya tathmini.


Afisa habari huyo wa Manispaa hakuweka wazi ingechukua siku, wiki au mwezi ili ikamilike na kutolewa taarifa kwa waandishi wa Habari.


Usiku wa kuamkia Julai 16, waandishi wa habari walifika katika kituo cha afya Sabasaba, ambapo mmoja wao alikuwa kama mgonjwa  na kukuta hali mbaya katika kituo hicho cha  sabasaba na  alilazimika kuzungumza  na mganga wa zamu Dk Facilius Zanzibar kuhusu hali iliyopo kituoni hapo.


Baadae mganga mfawidhi wa kituo hicho Dk Henry Mungia kufika  na kuwakuta wanahabari na kuhoji ruhusa ya  kuchukua Picha bila kibali, na alipotakiwa kuzungumza alikataa kurekodiwa kwa madai hadi apate ridhaa ya bosi wake ambaye ni mganga mkuu wa manispaa Dk Maneno ambaye naye licha ya kufika aligoma kuzungumza kwa kueleza kuwa watoa huduma kuachwe waendelee kuhudumia wagonjwa na angezungumzia suala hilo asubuhi ya siku inayofuata ambayo haikuwa na bila mafanikio


Wakati waandishi wa habari wanafika kituo cha sabasaba gari ya wagonjwa  halikuwepo, baadae ilifika saa saba usiku,.


Wagonjwa wa kuharisha na  kutapika walianza kuletwa kituoni hapo tangu saa nane mchana na baadae majira ya usiku ndipo walianza kuchukuliwa kupelekwa  kambi maalum ya wagonjwa wa kipindupindu eneo la mazimbu inayodaiwa ilikuwa imefungwa kwa kukosa wagonjwa siku za karibuni.


Baadhi ya wananchi waliozungumza na Mwandishi wa habari hizi walisema ni vyema uongozi wilaya ya Morogoro wakaendelea kutoa Elimu kwa wananchi juu ya tahadhali kwa kuzingatia usafi wa maeneo yao na chakula.


Mkazi wa kata ya Kichangani Joyce Mihambo alisema yeye bado hajasikia kama kuna ugonjwa wa kipindupindu lakini ushauri wake ni wananchi kuchukua tahadhali wakati wote kwa kuhakikisha wananawa mikoni na kuacha kula ovyo.


"Nazijua dalili za kipindupindu ni kuharisha wakati wote maji meupe na kutapika kama tutajilinda wenyewe kitaodoka,"alisema Joyce.


Naye Mussa Abbubakar, mkazi wa morogoro alisema ni vyema Elimu kwenye mitaa na kata kwa kutumia gari za matagazo ikaendelea  kutolewa na hata kupiga marufuku mikusanyiko isiyokuwa na lazima ambayo itasaidia kurudi hali ya kawaida.


Licha ya kituo cha afya sabasaba kupokea wagonjwa wanaosadikiwa kuwa wa kipindipindu mara kwa mara kutoka maeneo mbalimbali ya manispaa ya Morogoro, kituo hicho ndio limekuwa kimbilio kwa wagonjwa wengi wanaotoka pembezoni mwa Manispaa ya Morogoro kwa ajili ya kupata matibabu ya magonjwa mbalimbali ukiwemo kipindupindu.


Mmoja wa wauguzi ambaye hakutaka jina lake kuandikwa alimpozungumza na Mwandishi wa habari hizi Jana alieleza kuwa wagonjwa wa kuharisha maji meupe na kutapika mpaka kufikia julai 17 mchana walikuwa wamefikia 14.


Mwandishi wa habari hizi anaendelea kufatilia na kusubiri taarifa kutoka kwa mganga mkuu Manispaa ya Morogoro.


Mwezi Januari Mwaka huu katika Baraza la kawaida la madiwani Manispaa ya Morogoro, Meya wa Manispaa hiyo Paschal Kihanga alizungumza na kuwataka madiwani pamoja na watendaji wa Kata na Mitaa kuhakikisha wanaendelea kuwaelimisha wananchi kuhusu ugonjwa wa kipindupindu, hasa elimu ya kujikinga.


Mwisho.

No comments: