Mkataba wasainiwa kulindwa Shoroba ya Kwakuchinja - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Saturday 10 August 2024

Mkataba wasainiwa kulindwa Shoroba ya Kwakuchinja

 


Mkurugenzi msaidizi wa Idara Wanyamapori Eligi Kimario akiwa na Katibu wa Chem Chem Charles Sylivester baada ya kusaini Mkataba

Katibu Tawala msaidizi mkoa Manyara, Faraja Ngerageza




Afisa Wanyamapori mkoa Manyara Felix Mwasenga



Na: Mussa Juma, Babati


Maipacarusha20@gmail.com


Serikali imesaini mkataba wa kulindwa  eneo la mapito ya Wanyamapori (shoroba) la Kwakuchinja ambalo lipo kati kati ya hifadhi ya Taifa ya Tarangire na  Hifadhi ya Taifa ya Ziwa Manyara, ili kuzuia uvamizi wa eneo hilo na kupunguza migogoro baina ya wanyamapori na binaadamu.


Katibu Tawala msaidizi wa mkoa wa Manyara (Uchumi na Uzalishaji) Faraja Ngerageza  akizungumza na waandishi wa habari, baada ya kusainiwa mkataba huo,  baina ya Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia Idara ya Wanyamapori na Taasisi ya Chem Chem, amesema ushoroba huo  utatunzwa kutokana na umuhimu wake.


Ngerageza amesema Ushoroba wa Kwakuchinja una manufaa makubwa ya kiuchumi kwa mkoa wa Manyara na Taifa kwa ujumla hivyo lazima ilindwe na kutunzwa.


"Sisi mkoa tayari tumekamilisha taratibu zetu za kuhifadhiwa Shoroba hii, ili kuendelezwa shughuli za uhifadhi na Utalii  na tayari eneo limepimwa na mipaka yote imewekwa"amesema


Amesema mkoa kwa sasa unaendelea kutoa elimu kwa wananchi ambao wanaishi jirani na eneo hilo kufanya shughuli ambazo ni rafiki kwa shughuli za uhifadhi na Utalii.


Afisa Wanyamapori mkoa Manyara, Felix Mwasenga amesema na kilomita 137 ambalo ni shoroba kwa kuchinjwa tayari limebainishwa.


Mwasenga amesema eneo hilo linapatikana katika vijiji vya  Vilima vitatu, Kakoi, Minjingu na Olasiti.


Hata hivyo amesema katika eneo hilo asilimia 20.9 lipo katika vijiji na asilimia 116 lipo katika hifadhi ya jamii ya Burunge WMA.


Mkurugenzi msaidizi wa Idara Wanyamapori Eligi Kimario akiwa na Katibu wa Chem Chem Charles Sylivester wakisaini mkataba huo


Utiaji saini wa Mkataba


Awali, Akizungumza wakati wa kusainiwa mkataba huo, Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Wanyamapori, Eligi Kimario  amesema mkataba huo umesainiwa wakati muafaka ili kupunguza  migogoro baina ya wanyamapori na binaadamu katika eneo hilo.


Kimario amesema Ushoroba huu unahifadhiwa  kuruhusu wanyamapori kuvuka kutoka hifadhi na Tarangire na Kwenda Hifadhi ya Manyara na kurudi bila kusababisha migogoro.


Amesema kumekuwepo na migogoro katika eneo hilo hasa baada ya baadhi ya wananchi kujenga nyumba na kulima eneo la mapito ya wanyamapori.


Amesema katika mkataba huo,Taasisi ya Chem Chem inatarajiwa kuwajengea uwezo wa masuala ya uhifadhi watumishi ambao wanalinda ushoroba huo na pia kusaidia kulindwa.


Katibu wa Taasisi ya  Chem Chem, Charles Sylivester  amasema katika mkataba huo  wanatarajia kushirikiana na serikali kulinda na kuhifadhi shoroba ya kwakuchinja.


Anasema mkataba huo, utakuwa wa miaka mitano na unaweza kuendelezwa na utasaidia sana uhifadhi wa eneo hilo muhimu kwa sekta ya Utalii  na uhifadhi nchini.


Viongozi mbalimbali wameshiriki utiaji saini mkataba huu Jijini Dodoma wakiwepo viongozi wa Burunge WMA  na viongozi wa taasisi za uhifadhi.




MWISHO.

No comments: