Asasi za Kiraia zatoa Ilani ya Uchaguzi 2024/29 'Tanzania Tuitakayo' - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Friday 13 September 2024

Asasi za Kiraia zatoa Ilani ya Uchaguzi 2024/29 'Tanzania Tuitakayo'

 




Mussa Juma,maipac


maipacarusha20@gmail.com


Arusha. Asasi za Kiraia nchini zimezindua Ilani ya uchaguzi ya mwaka 2024/29 na kipaumbele cha kwanza ni kupatikana Katiba mpya.


Ilani hiyo imezinduliwa katika wiki ya asasi za kiraia mwaka 2024 ambayo imefanyika jijini Arusha.


Akizungumza katika uzinduzi wa Ilani hiyo, Mratibu wa mtandao wa watetezi wa haki Binaadamu (THRDC), Onesmo ole Ngurumwa alisema asasi za Kiraia zimetoa Ilani hiyo baada ya kukusanya taarifa na mahitaji katika jamii.


Amesema miongoni mwa mambo yaliyomo katika Ilani hiyo yanatarajiwa kuchukuliwa na vyama vya siasa katika kuandaa Ilani zao katika chaguzi zijazo.


Onesmo alisema Ilani hiyo ina vipaumbele vikubwa vitano na kwanza ni kupatikana Katiba Mpya ,kuwepo Uchumi jumuishi na maendeleo endelevu.


Jambo jingine lililopo katika Ilani hiyo ni kuwepo Usimamizi rasilimali na kupiga vita rushwa.


"Ilani hii pia imegusa masuala ya haki za binaadamu hasa na Utawala wa sheria lakini pia masula ya mazingira na mabadiliko ya tabia nchi"alisema


Alisema Ilani hiyo pia inataka uwepo wa tume huru ya uchaguzi kama msingi wa demokrasia.


"Asasi za kiraia pia zimeweza kutoa tunu za Taifa ambazo ni Amani, Utulivu, Umoja, Uzalendo kwa taifa, Lugha ya kiswahili na mengine kadhaa"alisema.


Wakizungumza baada ya kuzindua Ilani hiyo viongozi wa vyama vya siasa vya CCM, Chadema na CUF walipongeza Ilani hiyo.


Mjumbe wa Kamati kuu ya CCM, Rabia Abdalah na Mjumbe wa kamati kuu chadema, Godbless Lema walipongeza Ilani hiyo kwa kugusa mambo ya wananchi.


Rabia alisema CCM inathamini mchango wa CSOs katika kuchochea maendeleo katika taifa.


Alisema CCM, haijaliweka kando suala la Katiba mpya kwani bado linaendelea mchakato wa kupata Katiba mpya.


Lema alipongeza CSO kwa kazi kubwa ambazo inafanya na kuwataka viongozi kufika maeneo mbalimbali kutoa elimu ya uraia.


Alisema sasa taifa linapita katika wakati mgumu ikiwepo kuongezeka matukio ya utekaji ambayo yanaongeza hofu katika jamii.


Amesema taifa ambalo watu wake wanahofu linakosa ubunifu na uhuru wa kujieleza.


Akizungumzia Ilani hiyo, mwanaharakati wa katiba, Deus Kibamba alitaka vyama vya siasa kuchukuwa  ilani ya CSOs na kuifanyia kazi.


Alisema mengi yaliyoandikwa yanatokana na maoni ya wananchi waliowengi.


Mwisho

No comments: