BILIONEA MULOKOZI AJIANDIKISHA DAFTARI LA MPIGA KURA, AHIMIZA VIJANA KUJIANDIKISHA - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Sunday 8 September 2024

BILIONEA MULOKOZI AJIANDIKISHA DAFTARI LA MPIGA KURA, AHIMIZA VIJANA KUJIANDIKISHA


 



Na Mwandishi wetu, Babati


maipacarusha20@gmail.com 


Mkurugenzi wa kampuni ya vinywaji changamshi ya Mati Super Brand LTD, Bilionea David Mulokozi amewataka vijana nchini kujitokeza kwa wingi kujiandikisha kwenye uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura ili waweze kupiga kura kwenye chaguzi za serikali za mitaa na uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.


Mkurugenzi Bilionea Mulokozi ameyasema hayo leo Septemba 7 mwaka 2024 wakati akihakiki taarifa zake na kujiandikisha kwenye daftari la kudumu la wapiga kura.


Bilionea Mulokozi amesema vijana ndiyo nguvu kazi ya Taifa hivyo wajitokeze kwa wingi kutumia haki yao ya msingi katika kujiandikisha kwenye daftari la kudumu la wapiga kura na kushiriki katika uchaguzi.


"Mimi nimeshiriki leo hapa katika kituo cha kujiandikisha kilichopo kwenye shule ya sekondari Bagara hivyo natoa wito kwa vijana na wana Manyara kwa ujumla kushiriki kuhakiki taarifa zao," amesema Bilionea Mulokozi.


Amesema zoezi hilo halitumii muda mrefu hivyo vijana wasihofie hilo kwani inafanyika kwa njia ya kidigitali na inakamilika kwa muda mchache na kupatiwa kitambulisha chako papo hapo.


Amesema awali aliwahi kujiandikisha sehemu nyingine hivyo amehamisha taarifa zake kuja anapoishi hivi sasa kupitia daftari la kudumu la mpiga kura.


"Utaratibu umewekwa vyema na kila mlengwa unamuwezesha kujiandikisha na kuendelea na shughuli zake za uzalishaji mali na kujijenga kiuchumi," amesema Bilionea Mulokozi.


Hivi sasa kwenye mkoa wa Manyara, shughuli za kuhakiki taarifa za daftari la kudumu la wapiga kura zinafanyika kwenye wilaya za Babati, Hanang' na Mbulu, huku Wilaya za Simanjiro na Kiteto zikisubiria Septemba 25 mwaka huu.


MWISHO

No comments: