MAIPAC kuja na mkakati wa Kupaza Sauti, kuelimisha madhara ya Ukeketaji, LSF nao kuendelea kusaidia vikundi wanawake Longido - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Thursday 12 September 2024

MAIPAC kuja na mkakati wa Kupaza Sauti, kuelimisha madhara ya Ukeketaji, LSF nao kuendelea kusaidia vikundi wanawake Longido






Na: Mwandishi wetu, Longido


maipacarusha20@gmail.com 


Shirika la Wanahabari la usaidizi wa jamii za pembezoni (MAIPAC) linatarajia  kuzindua mradi kabambe  wa kuelimisha juu ya athari za ukeketaji kwa watoto wa kike katika jamii ya kifugaji ya kimasai ikiwa ni pamoja na kuwajengea wanawake uwezo wa kutetea haki zao.


Mradi huo unafadhiliwa na shirika la  Cultural Survival na unatarajiwa kusaidia pia kupaza sauti za vijana wanaopinga vitendo vya ukeketaji.


Mkurugenzi wa Shirika la MAIPAC, Mussa Juma ametoa taarifa hiyo katika ziara iliyofanywa na Asasi za kiraia katika wiki ya Asasi hizo iliyofanyika wilayani Longido.


"MAIPAC imebaini kuwa watoto wa miaka miwili hukeketwa kwa kificho katika Jamii ya Kimasai Wilayani Longido hivyo tunampango wa kuzindua mradi wa Kupaza Sauti na kuelemisha kuhusu masuala mazima ya ukeketaji na ukatili kwa watoto wa kike, lakini pia kuwajengea Uwezo wa kujiamini wanawake wa kimasai na kuweza kutetea haki zao za msingi hasa katika kukemea Ukatili" amesema.


Katika Ziara hiyo iliyofanywa na Asasi za kiraia (CSO) wadau wa asasi hizo wamepata wasaa wa kutembelea kikundi cha wanawake wanaofadhiliwa na shirika la Legal Service Facility (LSF) na Vodacom Foundation.


Akizungumza na ziara hiyo mkurugenzi wa LSF, Lulu Ng'wanakilala alisema shirika hilo limekuwa likisaidia vikundi 11 vya wanawake wa jamii ya kifugaji kata Kimokoa wilaya ya Longido.


Ng'wanakilala alisema  wanawake wa jamii za kifugaji bado wanakabiliwa na changamoto ikiwepo changamoto za kiuchumi, ushiriki katika siasa na changamoto za kiafya.


Hata hivyo alisema kupitia mradi wanaotekeleza longido wameweza kusaidia jamii ya wanawake kiuchumi kwa kuwa na miradi midogo, ushiriki katika masuala ya kisiasa na kupambana na changamoto za kiafya ikiwepo ukeketaji.


Wiki ya CSO hufanyika mara moja kila mwaka ambapo zaidi ya Wadau 600 wameweza kushiriki na kushirikishana Masuala mbalimbali ya kijamii kwa njia ya midahalo na Majadiliano ya kina yanayolenga Mchango wa CSOs hizo kwa maendeleo ya Taifa.






No comments: