RMO MIRERANI AWATAKA WACHIMBAJI KUWEKA MATENKI YA MAJI - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Wednesday 11 September 2024

RMO MIRERANI AWATAKA WACHIMBAJI KUWEKA MATENKI YA MAJI

 



Na Mwandishi wetu, Mirerani 


Afisa madini mkazi (RMO) Mirerani Nchagwa Chacha Marwa amewapa miezi miwili wamiliki wa migodi ya madini ya Tanzanite mji mdogo wa Mirerani wilayani Simanjiro mkoani Manyara, kuhakikisha kila mgodi unakuwa na matenki ya maji ili kuepuka maradhi ya vifua kwa wachimbaji.


RMO Nchagwa ameyasema hayo wakati akizungumza na wachimbaji wa madini ya Tanzanite juu ya usalama migodini.


Nchagwa akielezea kwenye kikao cha uchimbaji salama kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za madini, amesema baada ya miezi miwili ukaguzi utafanyika.


"Tunapaswa kuhakikisha kuwa kila mgodi unakuwa na tenki la maji lenye ujazo wa kuanzia lita 1,000 ili yatumike mgodini hasa wakati wa kuchoronga miamba ili kuondoka vumbi linalosababisha maradhi," amesema Nchagwa.


Amesema ni vyema wachimbaji madini wakachukua tahadhari kwa kuhakikisha wanatumia maji ili kuepusha maradhi yanayosababishwa na vumbi mgodini.


"Nategemea baada ya miezi miwili matenki yawepo na kila mgodi ufunge simu kutoka mgodini hadi juu ili kurahisisha mawasiliano pindi kukitokea tatizo," amesema Nchagwa.


Kaimu Mkurugenzi wa mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira Arusha (AUWSA) CPA John Ndetiko amesema wamejipanga kuhakikisha wanafikisha maji ndani ya ukuta wa madini ya Tanzanite na kuuza kwa bei nafuu.


CPA Ndetiko amesema wanatarajia kuuza maji lita 1,000 kwa shilingi 3,000 wakati wakifanya mikakati ya muda mrefu kufikisha maji ya bomba kwenye migodi ya madini ya Tanzanite.


Akizungumza na wadau hao wa madini Dk Alexander Mbuye anayejihusisha na udhibiti wa magonjwa ya kifua kikuu, maambukizi ya VVU na Silicosis migodini amesema maji ni muhimu kwenye uchimbaji.


"Njia pekee ya kuzuia kuvuta vumbi ili kuepuka Silicosis migodini ni kutumia maji mengi kwani ugonjwa hauna dawa baada ya mapafu kuathirika na vumbi," amesema.


Makamu Mwenyekiti wa chama cha wachimbaji madini mkoa wa Manyara (MAREMA) Tawi la Mirerani, Peter Loiting'id Laizer amesema suala la wachimbaji kuwa na tenki la maji lita 1,000 halina mjadala kwani ni kwa ajili ya manufaa ya wachimbaji madini.


"Kama nyumbani mtu na familia yake anakuwa na tenki la lita 3,000 kwenye machimbo ya madini ya Tanzanite pia inatakiwa awe na tenki la 1,000 ili kufanikisha uchimbaji salama," amesema.


Mwenyekiti wa mamlaka ya mji mdogo wa Mirerani, Adam Kobelo amesema wachimbaji wanapaswa kutekeleza suala la maji na kuweka simu kwa ajili ya mawasiliano mgodini.


Mchimbaji wa madini Zephania Joseph amesema anaunga mkono kuwepo na matenki ya maji kwa wachimbaji kwa ajili ya kuondoa vumbi mgodini baada ya kulipuliwa baruti.


MWISHO

No comments: