UNDP/SGP na TNRF wazinoa Taasisi zilizopata ruzuku - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Saturday 21 September 2024

UNDP/SGP na TNRF wazinoa Taasisi zilizopata ruzuku

 


Mratibu wa programu ya ruzuku ndogo za GEF wa, Faustine Ninga akifundisha asasi za kiraia zilizoata ruzuku hiyo jijini Dodoma

Washiriki katika picha ya pamoja 


Na: Mwandishi wetu, Maipac 


maipacarusha20@gmail.com


Dodoma.Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa(UNDP) kupitia programu ya ruzuku ndogo(SGP) ambayo inafadhiliwa na Mfuko wa mazingira duniani(GEF) wamewanoa watendaji wa asasi za kiraia zilizopata ruzuku 2024/25 kutekeleza vyema miradi na jinsi ya kuandika ripoti.



Katika mafunzo hayo ambayo yameratibiwa na Jumuiko na Maliasili Tanzania (TNRF), asasi hizo pia zimepewa mbinu ya kushirikisha jamii katika utekelezaji wa miradi yao ili kuleta matokeo chanya.


Akizungumza katika mafunzo hayo, Mratibu wa programu ya ruzuku ndogo za GEF wa UNDP, Faustine Ninga alisema lengo la mafunzo hayo ni hakikisha Asasi zilizopata ruzuku zinakuwa na uwezo wa kutekeleza vyema miradi  yao ili kuchochea maendeleo katika jamii.


Ninga alisema asasi za kiraia zinapaswa kuzingatia matakwa ya mkataba uliosainiwa kabla ya kupewa ruzuku, ikiwepo kuzingatia sheria katika manunuzi na utekelezaji wa mradi.


"Kila taasisi hapa imesaini mkataba na kuna maelekezo ya jinsi ya kutekeleza miradi hivyo tuzingatie mikataba na kama kuna changamoto yoyote, ikiwepo kuhamisha fungu la fedha, unapaswa kutoa taarifa"alisema


Ninga alisema Asasi hizo pia zinapaswa kuandika vizuri taarifa za utekelezaji wa mradi, taarifa ya fedha na taarifa ya matokeo katika mradi.


"Hizi taarifa ni muhimu sana kwetu katika kufatilia mradi lakini pia kuhakikisha malengo ya mradi yanafikiwa"alisema


Alisema taasisi ambazo zitatekeleza vyema miradi na kuleta matokeo chanya katika jamii zitakuwa na fursa ya kunufaika na miradi mingine ikiwepo kuunganishwa na taasisi nyingine.


"Kikubwa zaidi tujuwe malengo ya progamu hii ni  kusaidia taasisi ndogo kusaidia jamii lakini pia kuweza kukua na kuwa na uwezo wa kutekeleza miradi mikubwa"alisema.


Ninga alizitaka taasisi hizo kufanyakazi na vyombo vya habari kwa kutangaza matokeo ya miradi kwani kuna faida nyingi.


Mratibu huyo alipongeza Taasisi ya wanahabari ya  MAIPAC kwa kutumia vyema vyombo vya habari katika utekelezaji wa miradi na kuvutia taasisi nyingine kusaidia miradi ya kijamii.


Mkurugenzi wa MAIPAC Mussa Juma alieleza manufaa ya kutumia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii katika utekelezaji wa miradi na kushauri  asasi kuwa na website na akaunti  katika mitandao ya kijamii ili kuonesha kazi zao ndani na nje ya nchi.


Akizungumza katika mafunzo hayo, Mkurugenzi wa TNRF, Zakaria Faustine alisema wanaridhishwa na kazi nzuri ambazo zinafanywa na taasisi zote zilizopewa ruzuku.


Faustine alizitaka taasisi kuendelea kushirikiana na TNRF pale zinapopata changamoto lakini pia zizingatie mikataba.


"TNRF tunaamini miradi yote inayotekelezwa ina manufaa makubwa ya kijamii na italeta matokeo chanya"alisema.


Mfuko wa Mazingira Duniani(GEF) kupitia Programu ya Ruzuku Ndogo inayotekelezwa na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP)  umetoa zaidi ya sh  4.04  bilioni kwa mashirika yasiyo ya kiserikali zaidi ya 44 nchini ili kutekeleza miradi ya Uhifadhi wa Mazingira, Misitu, kuendeleza ufugaji nyuki, kutunza vyanzo vya Maji na uwezeshaji Jamii kiuchumi.


Mwisho.

No comments: