Askofu amgomea RC Makonda - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Wednesday 30 October 2024

Askofu amgomea RC Makonda

 

Mzee Augostino Nnko akizungumza na waandishi wa habari

 


Na: Mwandishi wetu, Arusha 


maipacarusha20@gmail.com



Askofu Mkuu  wa  Kanisa la International Evangelism Church, Eliudi Isangya amemgomea Mkuu wa mkoa Arusha, Paul Makonda kwenda ofisini kwake, kusuluhisha mgogoro wa kugombea Kanisa.


Askofu Isangya amekuwa na Mgogoro kwa Zaidi ya miaka 10 na baadhi ya wakazi wa eneo la Sakila, wilayani Arumeru,  wanaongozwa na Augustino Nnko,  wanaolalamika Askofu huyo, kuchukuwa kanisa lao na ardhi yao.


Kutokana na mgogoro huo, ambao umeanza kutishia amani katika eneo hilo, Mkuu wa mkoa Makonda alimwandikia barua Askofu huyo, kufika ofisini kwake ili kusuluhishwa mgogoro huo Octoba mwaka huu.


Hata hivyo, Askofu Issangya amegoma na kumwandikia barua Makonda Octoba 7, 2024 yenye kumbukumbu FNB.29/07/2030 kumweleza hatafika kwenye  shauri hilo ofisini kwa makonda.

 

Askofu Issangya katika barua hiyo, ameeleza kuwa Kanisa na eneo linalogombewa alipewa na  Emiliano Nnko  Mei 9,2014 ambaye alifariki  Agosti 28,2014 na tayari shauri hilo lilikwenda mahakamani na alishinda.



“Tangu eneo hili likabidhiwe kwa kanisa ni miaka 18 sasa  kwanini  kesi iamuliwe na mahakama alafu bado tunaanza tena kujaji maamuzi ya mahakama, kama kuna mahala hapako sawa Ofisi yako imuelekeze Augostino Nnko  jinsi ya kwenda mahakamani ili kupata haki anayotafuta”ilisomeka barua hiyo.


Katika barua hiyo, Askofu Issangya amemtaka  Makonda kuheshimu maamuzi ya Mahakama na yeye yupo tayari kurudi mahakamani lakini sio vinginevyo.


Hata hivyo, Akizungumza na waandishi wa habari, Nnko akiwa na baadhi ya wakazi wa Sakila, alisema anashangazwa na kiburi cha Askofu Issangya kugomea wito wa mkuu wa mkoa.


“Anaendelea kuonesha dharua kwa watu na viongozi kutokana na jeuri ya fedha zake wakati akijua si kweli kuwa alipewa ardhi na kanisa”alisema


Alisema kwa mujibu wa Katiba ya kanisa la Pentekoste  kifungu cha 10(d) mjumbe wa bodi ya wadhamini hana mamlaka ya kutoa mali za kanisa kwa mtu, bila idhini ya mkutano mkuu wa waumini na  kupata kura robo tatu ya waumini.


“huyu Eminiano ambaye anasema alimpa kanisa na ardhi sio kweli kwani Emiliano alihamia kwenye kanisa lake na hakuwa na hayo mamlaka ya kumpa eneo la kanisa lingine”alisema


Alisema  tayari shauri hilo lilifikishwa mahakamani na kubainika  taratibu zilikiukwa, Askofu Issangya kupewa kanisa  na katika maamuzi ya baraza la ardhi  maombi namba 224.2005 Mwenyekiti J,S Mgetta alitoa maamuzi eneo hilo ni mali ya Pentecoste na kuipa jukumu kampuni ya udalali ya majengo kulifungua kanisa hilo.


Hata hivyo, alisema Askofu Issangya aligomea uamuzi huo na kuendelea kulifunga kanisa hilo na kudai ni mali yake na baadae alilibadili na kulifanya sehemu ya madarasa.


Nnko alisema alifikisha tena shauri hilo, ofisi ya mkuu mkoa na mwaka juzi, pia  katika barua ya Katibu tawala mkoa Arusha, yenye kumbu kumbu namba FA.129/255/01/183 Mhina E.L aliagiza Askofu Issanya kukabidhi kanisa  hilo kwa kanisa la pentecoste.


“Mkuu wa mkoa  ameelekeza kukabidhi mara moja kanisa na ardhi   kwa kanisa la pentecoste  tawi la Sakila mara moja baada ya barua hii ili kuepusha uvunjifu wa Amani katika eneo hilo”ilisomeka barua hiyo.


Hata hivyo, Alisema Askofu huyo hadi sasa ameendelea kukaidi kukabidhi kanisa na badala yake amekuwa akiwafungulia kesi mbali mbali waumini wa kanisa la pentecoste wanaodai eneo lao na kukamatwa.


“Mimi nimekamatwa mara kadhaa na kufikishwa mahakamani na kunyimwa dhamana ili tu tuache kudai kanisa na ardhi na anajua eneo hilo kuna kaburi la baba yangu, hivyo hatutakuwa tayari kuachia eneo letu”alisema. 


End

No comments: