Na: Burhani Yakub, Tanga.
maipacarusha20@gmail.com
Kitendo cha wazazi kukwepa kufuatilia maendeleo ya kila siku ya watoto wao wawapo shuleni kimeelezwa kuwa kimechangia kwa kiasi kikubwa maadili ya wanafunzi wa kike kuporomoka na wengine kupata mimba.
Mkuu wa Wilaya ya Tanga,Jafary Kubecha amesema hayo wakati wa mahafali ya wahitimu wa kidato cha nne wa Shule ya Sekondari ya wasichana ya Al-Kheir ya Jijini Tanga.
Amesema baadhi ya wazazi wakishawapeleka shuleni watoto wao huendelea na majukumu yao ya kutafuta maisha kwa kudhani kuwa wamemaliza kulipa ada na mahitaji mengine hivyo hawana jukumu jingine.
"Ukilipa ada na mahitaji mengine usidhani kuwa umemaliza, wazazi tufuatilie maendeleo ya kitaaluma na miendendo ya kitabia ya watoto wetu wawapo shuleni...tushirikiane na walimu kufuatilia kwa sababu wengi wao huharibikia au wameharibikia shuleni"amesema Kubecha.
Ameupongeza uongozi wa shule ya wasichana ya Al-Kheir kwa kuongoza katika eneo la maadili na kufanya vizuri kwenye mithani ya kitaifa ya kidato cha nne na sita hususani masomo ya sayansi.
Mkuu wa shule hiyo,Sheha Ahmed Sheha amesema Al-Kheir Islamic Girls Sekondari ilianza mwaka 1999 kwa kidato cha kwanza na mwaka 2009 yakaanza rami kufundishwa kidato cha tano ambapo wahitimu wanaotarajiwa kufanya mtihani wa kitaifa wa kidato cha nne mwaka huu idadi yao ni 54.
"Wanafunzi wetu waliohitimu hapa na kwenda maeneo mbalimbali ndani na nje nchi tumekuwa tukirejeshewa taarifa kwamba wanaongoza kwa kulinda maadili...hili linatutia moyo kwamba kazi yetu ya kuwalea hapa shule inaakisi mema katika jamii"amesema Sheha.
Mkurugenzi wa Taasisi ya Direct Aid Society *Tanga,Sheikh* Ahmad Farhat ambayo inaendesha shule hiyo amesema kwa mkoa wa Tanga mbali ya Al-Kheir Girls Sekondari pia inamiliki shule ya wavulana ya Sekondari na msingi Pongwe na Shule ya msingi Mus-ab.
"Tumejikita pia katika sekta ya Afya ambapo tunatoa huduma katika kituo cha afya kilichopo Sahare pia tumekuwa tukioa matibabu bila malipo kwa njia ya Mobile Clinic na kuwatahiri watoto wadogo ,kituo cha kulea watoto yatima cha Pongwe na tunafadhili miradi ya ujasiliamali"amesema Farhat.
No comments:
Post a Comment