Unesco Tanzania yapongeza MAIPAC kushirikisha vyombo vya habari kusaidia jamii. - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Sunday, 13 October 2024

Unesco Tanzania yapongeza MAIPAC kushirikisha vyombo vya habari kusaidia jamii.




Mkuu wa Mawasiliano na habari wa UNESC0 -Tanzania, Nancy Angulo wa pili Toka Kulia, akiwa pamoja na watendaji wa taasisi ya Maipac, alipotembelea ofisini hiyo hivi karibuni 


Na: Mwandishi wetu.


maipacarusha20@gmail.com 


Taasisi ya wanahabari ya kusaidia jamii za pembezoni (MAIPAC) imepongezwa na Shirika la umoja wa Mataifa la  Elimu, Sayansi ma Utamaduni (UNESCO) kwa kutumia vyema vyombo vya habari katika shughuli za usaidizi wa jamii za pembezoni.


MAIPAC imekuwa na mradi wa kupaza sauti kupinga ukeketaji, ukatili dhidi ya walemavu, wanawake na watoto wilaya ya Longido na mradi wa uhifadhi wa mazingira kwa maarifa ya asili na kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi katika wilaya za Monduli, Longido, Karatu na Ngorongoro.


Taasisi ya MAIPAC pia imekuwa ikitoa elimu ya kuhamasisha wananchi kujiandikisha katika daftari la kudumu la wapiga kura  baada ya kupewa kibali na tume huru ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na katika utekelezaji wa miradi hii imekuwa ikifanyakazi na vyombo vya habari zikiwepo radio za kijamii.

Mkuu wa Mawasiliano na habari wa UNESC0 -Tanzania, Nancy Angulo akizungumza na Mkurugenzi Mtendaji wa Maipac, Mussa Juma alipotembelea ofisini hapo


Mkuu wa  Mawasiliano na habari wa UNESC0 -Tanzania, Nancy Angulo akizungumza na wafanyakazi  baada ya kutembelea ofisi za MAIPAC alisema amefurahishwa na jinsi MAIPAC inavyotumia vyombo vya habari kutekeleza miradi yake.


Alisema MAIPAC ndio taasisi pekee  ya waandishi wa habari nchini ambayo inafanyakazi na jamii za pembezoni moja kwa moja .


"Nawapongeza MAIPAC mnafanya kazi nzuri na muendelee kufanyakazi na radio za kijamii na wanahabari kusaidia jamii"alisema


Alisema MAIPAC pia inapaswa kusaidia kuelimisha kupinga matukio ya ukatili dhidi ya walemavu, wanawake na watoto katika jamii.


"Kuelekea uchaguzi mkuu ni vyema katika kazi zenu kuzingatia maoni ya makundi yote ya jamii wakiwepo watu wenye ulemavu na wanawake"alisema


Angulo pia alipongeza  mpango kazi wa MAIPAC juu ya kuongeza ushiriki na Utetezi wa watu wenye ulemavu,wanawake na watoto katika masula kadhaa na kijamii.


Awali, Mkurugenzi mtendaji wa MAIPAC Mussa Juma na Meneja utawala  wa MAIPAC ,Andrea Ngobole waliomba UNESCO  kushirikiana na MAIPAC katika miradi yake kadhaa hapa nchini.


Juma alishukuru UNESCO kwa kuwaalika watendaji wa MAIPAC katika mafunzo juu ya masuala ya jinsia, utetezi na ushiriki wa watu wenye ulemavu,wanawake na watoto.


"Tumejifunza mengi na tunaimani kutumia elimu vizuri ikiwepo kuandaa vipindi maalum, makala na machapisho kuhamasisha ushiriki sawa wa watu wenye ulemavu,wanawake katika jamii pia kupinga ukatili dhidi ya watoto"alisema Musa


Katika mafunzo hayo pia mkuu wa kitengo cha mahusiano na habari cha Shirika la Umoja wa Mataifa la kusaidia Watoto Duniani (UNlCEF) Usia Nkhoma alitoa mada kuhusiana na muongozo kwa kufanyakazi na watoto ili kuepuka kuvunja sheria lakini kutowaumiza watoto.


Ngobole alisema MAIPAC itaendelea kufanyakazi kwa weledi katika kufanya utetezi na uchechemuzi wa mambo ya kusaidia jamii.


Naye Meneja wa miradi wa MAIPAC, Ramadhani ulenje alisema MAIPAC bado inahitaji ushirikiano na wahisani na wadau mbalimbali katika kutekeleza Miradi yake.


Ulenje alishukuru UNESCO kuwapa fursa ya mafunzo na kuahidi yale yote waliyokubaliana watatekeleza katika mpango kazi wao.


Taasisi ya  Wanahabari ya MAIPAC imekuwa ikifanya kazi na mashirika kadhaa  ikiwepo  Mfuko wa Mazingira Duniani(GEF) kupitia Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) Shirika la kimataifa Cultural Survival, Foundation for Civil Society (FCF), PINGOs Forum, THRDC, Jumuiko la Maliasili Tanzania (TNRF) na Serikali.



No comments: