Na Prisca Libaga Maelezo Arusha
maipacarusha20@gmail.com
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) itahakikisha wananchi wengi wanafikiwa na huduma za kibingwa za uchunguzi na matibabu ya moyo kupitia program yake ya tiba mkoba ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hasssan.
Hayo yamesemwa leo jijini Arusha na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi hiyo Dkt. Peter Kisenge wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu kambi maalumu ya uchunguzi na matibabu ya moyo inayofanyika Arusha Lutheran Medical Center.
Dkt. Peter Kisenge alisema kufanyika kwa kambi hiyo kunatokana na kambi ya uchunguzi na matibabu ya magonjwa ya moyo iliyofanyika mwezi wa sita mwaka huu jijini Arusha.
Dkt. Kisenge alisema wamerudi tena mkoani Arusha kufanya kambi ya uchunguzi na matibabu ya moyo ili kuwapima watu wenye matatizo ya moyo na kutoa elimu ya magonjwa yasiyoambukiza ambapo watu 200 sawa na asilimia 30 ya watu waliojiandikisha kwa siku mbili wamegundulika kuwa na magonjwa ya moyo.
“Kambi ya kwanza tuliyoifanya Arusha tuliona watu 1350 tuliowakuta na matatizo ambao ni watu wazima walikuwa asilimia 14 na watoto asilimia tisa, sasa hivi asilimia imekuwa 18 ni kubwa ukilinganisha na wakati ule hii inatokana na tunaowaona hivi sasa wengi wao ni wagonjwa na wakati ule tuliona wasio wagonjwa na wagonjwa”.
“Vitu vinavyosababisha magonjwa ya moyo ni pamoja na unywaji pombe kupitiliza, kutokula vyakula bora, kutokufanya mazoezi na uvutaji wa sigara hivyo ni vizuri wananchi wafanye mazoezi ili kupunguza kupata magonjwa yasiyoambukiza yakiwemo ya moyo”, alisema Dkt. Kisenge.
Alisema sababu ya pili ya kwenda Arusha ni mkoa wa utalii wanaimarisha afya ya utalii kwa watalii, watatoa elimu kwa wataalamu wa afya waliopo katika hospitali za Mt. Meru, Arusha Lutheran Medical Centre na Arusha International Conference Centre (AICC) ili waweze kutoa huduma za kibingwa za matibabu ya moyo kwa wananchi wa mkoa huo.
Dkt. Kisenge ambaye pia ni daktari bingwa wa magonjwa ya moyo na mishipa ya damu aliwaomba wananchi kujiunga na bima ya afya kwa wote pindi itakapoanza kwani gharama ya matibabu ya moyo ni kubwa lakini kama mtu akiwa na bima ya afya itampunguzia gharama ya kulipia matibabu hayo.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Arusha Lutheran Medical Center Dkt. Goodwill Kivuyo aliwashukuru wataalamu wa JKCI kwa kufanya kambi ya matibabu ya moyo katika hospitali hiyo ambayo imewasaidia wananchi kupata huduma pamoja na kuwajengea uwezo wataalamu wa afya wa hospitali hiyo.
Dkt. Kivuyo ambaye ni bingwa wa upasuaji aliishukuru serikali kwa kuweka mwongozo na makubaliano ya taasisi za umma hasa za hospitali ya kuanzisha mahusiano na hospitali binafsi jambo lililosababisha wananchi wengi zaidi kupata huduma za matibabu ya kibingwa.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment