JUKWAA LA JAMII SULUHU YA MIGOGORO KWA WANANCHI, NA KUPATA FURSA - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Tuesday, 8 October 2024

JUKWAA LA JAMII SULUHU YA MIGOGORO KWA WANANCHI, NA KUPATA FURSA

 




Na Lilian Kasenene, Morogoro


maipacarusha20@gmail.com


IMEELEZWA uwepo wa Jukwaa la Jamii kila mwezi linaloandaliwa na Kituo cha Msaada wa Sheria Morogoro(MPLC) limesaidia kutatuliwa kwa changamoto mbalimbali za kisheria pamoja na wananchi kupata fursa na elimu inayochangia kuchochea maendeleo ndani ya jamii.


Jukwaa la Jamii ni jukwaa lililoanzishwa na MPLC  kwa lengo la kuwakutanisha wadau na wananchi wa Manispaa ya Morogoro kuweza kukutana na kutatua changamoto,kujifunza na kupeana fursa zikiwemo za kiuchumi na kisheria.


Wadau mbalimbali wamezungumza na Mwandishi wa Habari hii mjini Morogoro kwa nyakati tofauti.


Ndege Magoma mkazi wa Morogoro anasema wananchi wengi hawana uelewa wa mambo ya kisheria pindi wanapopatwa na shida na hawajui njia sahihi ya kupata elimu ya kisheria,lakini toka lilipoanzishwa jukwaa hilo la jamii mwezi juni kumekuwa na mabadiliko ndani ya jamii.


Magoma anasema ushiriki wa wananchi katika Jukwaa hilo,na kuwasilisha changamoto zao za kisheria na masuala mengine kumewafanya kubadilika na kujua nini wanapaswa kufanya ili kukabiliana na changamoto za kisheria zinazowakabili.


“Nimeshiriki Jukwaa la Jamii toka lilipoanzishwa na MPLC kwa kushirikiana na mashirika mengine,nimepata uelewa mkubwa katika nyanja zima ya kisheria na masuala ya mazingira,hivyo nawasihi wananchi tushiriki  kwa wingi kwani kuna fursa nyingi za kujenga,”anasema Magoma.


Naye Mariam Mussa anasema Jukwaa la Jamii limekuja kwa wakati katika manispaa ya Morogoro kwani wakina mama walikua wanakosa sehemu za kupata elimu ya ujasiriamali na wale ambao tayari wajasiriamali wamepata sehemu kutangaza na  kuuza bidhaa zao kwa urahisi.


Anasema jukwaa litaleta mabadiliko na kukuza uchumi wa wajasiriamali wadogo kwani kila linapofanyika Jukwaa la Jamii kuna wataalamu wa wanatoa elimu za ujasiriamali na namna ya kuweza kuboresha biashara na kuongeza kipato.


“Kila ninaposhiriki Jukwaa la Jamii naondoka na kitu kipya kichwani cha kuweza kubadili maisha yangu na kuaacha kuishi kimazoea, nilikuwa muoga sana kufanya biashara lakini hivi sasa niko tayari kuanzisha biashara na kuondokana na utegemezi,"anasema Mariam.


Mkurugenzi wa Taasisi ya Tanzania Albinism Society(TAS) Morogoro Hassani Mikazi anasema Jukwaa la Jamii limekuwa msaada mkubwa kwa jamii,kwani ushiriki wananchi umekua ukiongezeka na wadau ambao wanataka kutumia jukwaa hilo kutoa elimu na kutangaza kazi zao wanaongezeka kila wakati.


“Nimekuwa mmoja wa waandaji wa Jukwaa la Jamii toka lilipoanzishwa,naona ushiriki umekua mkubwa kwa wananchi na hii ni dalili nzuri kuwa wananchi wana kiu ya kubadili fikra zao,na kutumia Jukwaa ni sehemu ya maisha yao ya kujifunza na kupata fursa,”anasema Mikazi


Mratibu wa Jukwaa la Jamii, Msaidizi wa Kisheria kutoka MPLC l Chediel Senzighe anasema Jukwaa la Jamii limeweza kutoa msaada wa kisheria kwa wananchi zaidi ya 200,ambao walikua na mashauri tofauti tofauti.


Senzighe anasema Jukwaa la Jamii ni uwanja huru,ambao kila mwanachi anaruhusiwa kushiriki kwa lengo la kujifunza na kupata fursa mbalimbali,kwani siku ya Jukwaa la Jamii kuna mjumuiko wa wataalam mbalimbali hivyo mtu akishiriki lazima aondoke tofauti na alivyokuja.


Mwisho.

No comments: