Mtoto auwa kikatili Arusha,wananchi wavunja nyumba ya watuhumiwa,polisi watoa tamko - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Sunday, 13 October 2024

Mtoto auwa kikatili Arusha,wananchi wavunja nyumba ya watuhumiwa,polisi watoa tamko

 



Wakazi wenye Hasira Kali walivyovamia Nyumba



Na: Mussa Juma, Maipac 


maipacarusha20@gmail.com 


Ni tukio la aina yake limetokea katika eneo la Kata ya Murieti kwa Mrombo, baada ya kuuawa kikatili kwa kutenganishwa viungo Mtoto, Mariam Khatibu(11)


Mwili wa Mtoto huyo, umebainika, ukiwa umewekwa kwenye beseni, baada ya kusambaa taarifa za kupotea Mtoto huyo ambaye alikuwa ametumwa dukani majira ya asubuhi.


Kamanda wa polisi mkoa Arusha, Justine Masejo  October 13, 2024 amethibitisha kutokea kwa tukio hili la aina yake na kueleza uchunguzi umeanza.


Kamanda Masejo amesema  Polisi Mkoa wa Arusha tayari linawashikilia wanandoa wawili ,Jaina Mchomvu(50) na Ramji Hatibu Mlacha(60) wakituhumiwa kuhusika na  kumuua kwa kumchinja Mtoto mwanafunzi wa darasa la Sita wa shule ya Msingi Domino, Mariam Juma khatibu(11) mkazi wa kwa Mrombo katika jiji la Arusha.


Tukio hili la ukiukwaji wa Haki za watoto  linalohusishwa na imani za ushirikina.


Mmoja wa mashuda wa tukio hili Regina Peter amesema mwili wa marehemu ulikutwa mchana saa sita chini ya uvungu wa kitanda ukiwa umekatwakatwa vipande na kuwekwa kwenye beseni baada ya mjukuu wa mtuhumiwa kuona mkono wa marehemu ukining'inia wakati akitafuta kiatu .


Amesema Mtoto huyo kabla ya kifo chake  alikuwa ametumwa dukani toka asubuhi lakini hakurejea na ilipofika mchana wazazi wake walianza kumtafuta maeneo mbalimbali baada ya kuingiwa na wasiwasi.


Kamanda Masejo amesema hadi sasa watu watatu wanashikiliwa akiwemo mshukiwa namba moja Jaina Mchomvu ambaye amekamatwa na askari Polisi huko Mabogini Moshi, Mkoani Kilimanjaro alikokimbilia kujificha baada ya kutenda tukio hilo.


Kamanda Masejo amesema kuwa Baada ya kukamatwa kwa mtuhumiwa, Jaina Mchomvu alihojiwa na kukiri kutenda tukio hilo la mauaji ya mtoto huyo.


Kamanda Masejo alifafanua kuwa Uchunguzi wa tukio hilo unaendelea kwa kushirikiana na mamlaka mbalimbali za kiuchunguzi ili kubaini chanzo cha tukio hilo.


Hatibu Mlacha  siku ya tukio aliondoka kusikojulikana na alimpigia simu mtoto wake wa kike aitwaye Ramji na kumwagiza aende nyumbani kwake kumsaidia kufua.


Taarifa zimedai kuwa Ramji alifika nyumbani kwa mtuhumiwa (Mama yake) akiwa na mtoto wake na wakati akiendelea na shughuli za usafi ghafla  mtoto wake aliyekuwa akitafuta kiatu chini ya uvungu alimwambia ameona mkono wa mtu chini ya uvungu kwenye beseni.


Ramji ambaye pia anashikiliwa na polisi aliingia ndani na kushuhudia mkono wa mtu na kuanza kupiga kelele ndipo wananchi walipojitokeza na baadaye polisi walifika eneo la tukio na kuondoka na mwili wa marehemu. 


Katika hatua nyingine wananchi wenye hasira kali wamebomoa nyumba yote ya mtuhumiwa na kuisambaratisha  na kisha kuteketeza kwa moto vitu mbalimbali zikiwemo nguo huku baadhi ya vitu vyake vikiporwa.


Mwili wa marehemu unatarajiwa kuzikwa  baada ya kukamilika shughuli za kiuchunguzi.


Tukio limekuja wakati kukiwa na ongezeko la watoto kupotea katika maeneo mbalimbali nchini matukio yakihusishwa na ushirikina.


Mwisho


 

 

No comments: