Na Julieth Mkireri , MAIPAC KIBAHA
maipacarusha20@gmail.com
ZAIDI ya wakazi Miln 1.2 Mkoani Pwani wanatarajiwa kuandikishwa kwenye daftari la kudumu la mpiga kura uandikishaji unaoanza leo hadi Oct 20 .
Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge ameyasema hayo alipokuwa akizindua uandikishaji huo katika Mtaa wa Mkoani kata ya Tumbi Halmashauri ya Mji wa Kibaha.
Akizungumza na Waandishi baada ya kujiandikisha Kunenge amesema wananchi wanatakiwa kujitokeza kujiandikisha Ili waweze kuwa na haki ya kuchagua viongozi wanaowataka kwenye ngazi za Vijiji na Mitaa.
" Maendeleo siku zote yanaanzia ngazi za chini na uchaguzi huu unahusu viongozi wa nafasi hizo kabla ya uchaguzi mkuu ujao hivyo wananchi mnatakiwa kutumia nafasi yenu kujiandikisha Ili muweze kuchagua viongozi mnaowataka watakaowasemea matatizo yenu," amesema Kunenge.
Kunenge amebainisha kuwa Mkoa huo umetenga vituo 2374 vya kujiandikishia na kwamba wamelazimika kutenga vituo vingi Ili kupunguza msongamano na kuwarahisishia wananchi kuvifikia kwa urahisi.
Mmoja wa wananchi waliojitokeza kujiandikisha Emmanuel Masele mkazi wa mtaa wa Mkoani A amesema ni vema wananchi wakajiandikisha kwa wingi Ili waweze kuchagua kiongozi wanayemtaka na kuondoa malalamiko .
Mkoa wa Pwani una Vijiji 417, Mitaa 73 na Vitongoji 2028 na kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022 Mkoa huo una wakazi 2,024.949 wakiwa wanawake 990,616 na Wanaume 1,026,331 .
Mwisho
No comments:
Post a Comment