Wananchi Babati Waaswa Kudumiaha Amani na Usalama - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Friday, 11 October 2024

Wananchi Babati Waaswa Kudumiaha Amani na Usalama

 


Na Epifania Magingo,Manyara 


maipacarusha20@gmail.com 


Wananchi Wilayani Babati Mkoani Manyara wameaswa kudumisha amani na usalama hasa kwenye kipindi hiki cha kuelekea kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa ili kila mwananchi aweze kutimiza haki yake ya kikatiba ya kuchagua viongozi wa kijiji, kitongoji na mtaa kwaajili ya maendeleo endelevu ya Taifa la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.


Uchaguzi wa Viongozi wa Serikali za Mitaa utafanayika 27 November 27 ,2024 huku ikitajwa kuwa zoezi la kujiandikisha kwenye daftari la wakazi la mpiga kura linaanza 11 Octoba hadi 24 octoba ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya Uchaguzi wa Viongozi hao.


Hayo yamezungumzwa na Mkuu wa Wilaya ya Babati Emmanuela Mtatifikolo Kaganda ofisini kwakwe na kusisitiza kuwa amani na usalama vikitoweka, itawakosesha wananchi fursa adhimu ya kuchagua viongozi wanaowataka lakini pia itaharibu sifa nzuri ya amani ya nchi yetu.


“Nitumie fursa hii kuomba na kuelekeza kwamba tunaingia kwenye zoezi muhimu sana, sitarajii kuona kikundi chochote au mwananchi yeyote akijitokeza na kutaka kuvuruga zoezi hili la uandikishaji au zoezi zima la upigaji kura kwenye eneo letu, tunatamani kuwa na wakati mzuri wenye utulivu ili kila mmoja aweze kutumia nafasi hii kwenda kujiandikisha.”


Aidha ,Kaganda amesema  kuwa endapo kitaonekana kiashiria chochote cha uvunjifu wa amani wakati wa zoezi la uandikishaji na zoezi la uchaguzi, wananchi watoe taarifa kwenye vyombo vya usalama ili jambo hilo liweze kushughulikiwa haraka iwezekanavyo.


“Yeyote atakayeona kuna viashiria vya uvunjifu wa amani au harakati zozote ambazo hazina afya ndani ya wilaya yetu atoe taarifa haraka ili lishughulikiwe, kama mwenyekiti wa kamati ya usalama ya wilaya natamani sana tuwe na kipindi kizuri, tuwe na utulivu ili kila mwana Babati mwenye sifa asiwe na kikwazo chochote cha kwenda kujiandikisha.”


Kuhusu mkanganyiko wa zoezi hili ambao umejitokeza kwa wananchi juu ya tofauti ya kujiandikisha kwenye daftari la kudumu la mpiga kura na daftari la makazi Kaganda amesema daftari la makazi ni maalum kwaajili ya uchaguzi wa serikali za mitaa na ndilo litakalowawezesha wananchi kuchagua viongozi wao kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa lakini daftari la kudumu la mpiga kura ni maalum kwa uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 utakaohusisha madiwani, wabunge pamoja na Rais.

No comments: