CHADEMA SIMANJIRO WAFURAHIA WAGOMBEA WAO KUTOKATWA - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Sunday, 10 November 2024

CHADEMA SIMANJIRO WAFURAHIA WAGOMBEA WAO KUTOKATWA

 



Na Mwandishi wetu, Simanjiro 


maipacarusha20@gmail.com 


CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo na Maendeleo CHADEMA Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, kimewapongeza wasimamizi wa uchaguzi kwa kutenda haki na kuwapitisha wagombea uenyekiti wa vitongoji na vijiji bila kukata majina yao.


Katibu mwenezi wa CHADEMA Wilaya ya Simanjiro Ambrose Ndege ameeeleza kuwa wanatarajia kuanza kufanya kampeni ya uchaguzi November 20 kwenye maeneo mbalimbali.


"Tunawashukuru viongozi wa Wilaya Simanjiro na kata zote za mji mdogo wa Mirerani kwa kutenda haki bila kubagua au kukata majina ya wagombea wetu," amesema Ndege .


Amesema anaishukuru TAMISEMI kwa kuweka viongozi makini Wilaya ya Simanjiro, kata zote na mamlaka ya mji mdogo wa Mirerani kwani wamesimamia mchakato wa uchaguzi vyema na sasa wanasubiria kuanza kampeni muda utakapofika.


"Wagombea wote kwenye maeneo tuliyowasimamisha wamepitishwa hakukuwa na vikwazo vya fomu kukosewa au mizengwe yoyote timetendewa haki watu waingie uwanjani wanadi sera zao wapigiwe kura na siyo kupita bila kupingwa," amesema Ndege.


"Tangu mwaka 2014 hatujafanya uchaguzi wa halali Simanjiro kwani wagombea wetu wamekuwa wakienguliwa ila mwaka huu wa 2024 tunawapongeza viongozi wa Serikali kwa kutekeleza vyema wajibu wao," amesema Ndege.


Amesema kwenye mji mdogo wa Mirerani wamefanikiwa kusimamisha wagombea uenyekiti kwenye vitongoji 23 kasoro kitongoji kimoja.


"Huyu mgombea wa Zaire ameandika barua mwenyewe ya kutogombea ila hakukatwa jina lake ameamua mwenyewe hatufahamu kilichomsibu," amesema Ndege.


Mwanachama wa CHADEMA Adam Woiso amesema wasimamizi wa uchaguzi wamefanya vyema kwani jamii inapaswa kufanya uchaguzi kwa kuchagua wagombea kupitia vyama na siyo kuwapitisha bila kupingwa.


"Kwa hapa wasimamizi wa uchaguzi wanastahili pongezi kwani wametekeleza wajibu wao ipasavyo na sisi tunajipanga vyema kwenye maandalizi ya kufanya kampeni," amesema Woiso.


MWISHO

No comments: