Kamati ya Bunge ya Maji na Mazingira yaridhishwa kurejeshwa maji safi na salama Kwa walioathiriwa na maporomoko Mlima Hanang' - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Sunday, 10 November 2024

Kamati ya Bunge ya Maji na Mazingira yaridhishwa kurejeshwa maji safi na salama Kwa walioathiriwa na maporomoko Mlima Hanang'




Na Epifania Magingo,Manyara.

maipacarusha20@gmail.com

Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Maji na Mazingira imeridhiahwa na mpango wa kurejesha huduma ya maji safi na salama katika maeneo yaliyoathirika na maporomoko ya tope Wilaya ya Hanang Mkoani Manyara.


Mwenyekiti wa Kamati hiyo Jackson Kiswaga ameyasema hayo wakati wa ziara ya kutembelea maeneo ambayo yaliathiriwa na maporomoko ya tope Wilayani Hanang Mkoani wa Manyara.


Amesema wamejionea na kuridhishwa na kazi ya kurejesha miundombinu ambayo imefanywa kwa haraka kupitia Bilioni 9 zilizotolewa na Serikali.


"Ari na kasi ya utendaji kazi iendelee tunataka azma ya Rais Dokta Samia Suluhu Hassan ya upatikanaji wa maji safi na salama ya kufikia asilimia 85 Vijijini na asilimia 95 mijini itimie ifikapo 2025"


Kwa kujibu wake kamati itakwenda kusukuma fedha katika miradi ambayo imeshaanza lakini haijapata fedha ili iweze kukamilika kwa wakati.


Ziara ya kamati hiyo imetokana na maombi ya Mbunge wa Jimbo la Hanang Samwel Hhayuma ya kuitaka kamati kuona hali ya huduma ya maji katika maeneo yaliyoathirika na maporomoko ya tope na mpango wa kurejesha huduma ya maji Wilayani Hanang.


Amesema Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dokta Samia Suluhu Hassan imekuwa nyepesi katika kupeleka fedha kwenye miradi kuanzia kwenye vijiji,kata,wilaya hadi mkoa zinazotekeleza miradi.


Awali, Naibu Waziri wa Maji Mhandisi Kundo Mathew amesema zaidi ya miradi minne ya maji iliharibiwa Wilayani Hanang na miradi miwili katika mji wa Katesh kufuatia maporomoko ya tope.


Wizara ya maji ilikuja na mpango wa dharura wa kuhakikisha inapatikana njia ambayo wananchi walioathiriwa wanapata maji.


"Sambamba na adha hiyo nalipongeza sana Bunge tumepitia mpango wa dira ya Taifa ya mwaka 2050 hiyo ndio dira ambayo itaenda kubainisha mipango ya wizara ya maji hivyo tumeendelea kutekeleza miradi ya kimkakati".


Amesema Sekta ya maji kupitia Waziri wa Maji Jumaa Aweso imeendelea kuhakikisha miradi ya kimkakati ya kuvuta maji kutoka ziwa Victoria lakini na matumizi ya maji kutoka ziwa Tanganyika pamoja na kutumia vyanzo vingine vya maji vya mabwawa ili kusambaza maji kwa wananchi walio wengi nchini.


Mkuu wa Mkoa wa Manyara Queen Sendiga amesema kuwa Mkoa umefanya kazi nzuri ya utekelezaji wa miradi ya maji tangu Rais Samia alipoingia madarakani ambapo upatikanaji wa maji safi na salama kwa wananchi umeongezeka na kufikia mijini asilimia 84 na vijijini asilimia 71.


Amesema kuwa Manyara ni Mkoa wenye asili ya kifugaji na baadhi ya maeneo ni kame ambayo hayapatikani maji kwa urahisi hivyo kupitia miradi ya maji inayotekelezwa inasaidia upatikanaji wa maji safi na salama.


Akitoa taarifa ya Mkoa kuhusu huduma ya maji Meneja wa Wakala wa maji mjini na vijijini (RUWASA) Mkoa wa Manyara James Kionaumela amefafanua kuwa mpango wa dharura ,wa muda mfupi na muda mrefu ulitumika kurejesha huduma ya maji katika maeneo yaliyoathiriwa na maporomoko.


Mpango huo ni pamoja na uchimbaji wa visima virefu 15 ambapo visima 9 vikipata maji na 6 haikupata maji.

No comments: