Madaktari Bingwa Waweka Kambi ya Matibabu Mkoani Manyara - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Tuesday, 19 November 2024

Madaktari Bingwa Waweka Kambi ya Matibabu Mkoani Manyara


Mkuu wa Mkoa wa Manyara Queen Sendiga

Mkuu wa Mkoa wa Manyara Queen Sendiga


 Na Epifania Magingo, Manyara.


Timu ya Madaktari Bingwa na wabobezi wa Afya ya binadamu Mkoani Manyara wameandika historia kwa kuanza kutoa kliniki ya kwanza ndani ya Mkoa huo ya magonjwa mbalimbali kutokana na kuwepo kwa vifaa tiba vya kutosha.


Katika kufikia malengo ya mpango mkakati wa Taifa wa Afya kwa wote ifikapo mwaka 2030 kliniki za Madaktari Bingwa  na wabobezi zimekuwa zikifanyika nchi nzima ambapo Mkoa wa Manyara kupitia Madaktari Bingwa  na wabobezi walioko Mkoani humo wamezindua mpango wa kutoa huduma ya magonjwa mbalimbali.


Akizungumza na waandishi wa Habari wilaya ya Babati Mkoa wa Manyara, Mkuu wa Mkoa wa Manyara Queen Sendiga amesema mpango huo  umezunduliwa katika wilaya ya Simanjiro ambapo  madaktari bingwa na wabobezi 15 watatoa huduma kuanzia tarehe 19 hadi 22 mwezi Novemba mwaka 2024 .


"Wanakwenda kuweka kambi katika wilaya moja ili wananchi wote wanaohitaji huduma ya kibingwa na kibobezi waweze kupata tiba kutokea kwenye eneo hilo na kuhamia katika wilaya zingine mkoani humu".


Amesema hatua hiyo inaunga mkono wazo lililobuniwa na Rais Dokta Samia Suluhu Hassan kwa lengo la kuwapatia wananchi wote huduma za kibingwa bobezi katika magonjwa mbalimbali yanayowakabili katika maeneo yao.


Aidha ,amesema mpango huo unalenga pia kupunguza gharama za wananchi kusafiri kwenda kufuata huduma za kibingwa na kibobezi katika mikoa mingine pamoja na gharama za kuwaona Madaktari Bingwa  na wabobezi hao.


Pia,amesema utafanyika uchunguzi wa awali wa magonjwa mbalimbali kabla ya kuwa sugu, kuwajengea uwezo watumishi wa Afya kupitia Madaktari Bingwa na wabobezi wa Mkoa pamoja na kufahamu uhalisia wa magonjwa katika eneo husika.


Queen Sendiga amewataka wananchi kujitokeza kwa wingi kupata tiba na ushauri wa magonjwa mbalimbali kupitia fursa ya uwepo wa Madaktari Bingwa na wabobezi wa Mkoa.


Àmetoa ufafanuzi kuwa Madaktari hao  ni waajiriwa wa Serikali ambao wamepangiwa kufanyakazi Mkoani Manyara ambapo amekiri uwepo wao na kueleza kwamba watatumia vifaa tiba vya kisasa vilivyopo katika hospitali ya Mkoa, Wilaya na Rufaa kutoa tiba endelevu.


"Kwa kuwa vifaa tiba tunavyo na madaktari bingwa na wabobezi tunao tumeona hakuna sababu ya kuendeleza,kusubiri ratiba ya madaktari bingwa na wabobezi ya kitaifa wapite sisi tunaanza na madaktari bingwa tulionao ndani ya mkoa kuunga juhudi za Rais Dokta Samia Suluhu Hassan" .


Amesema magonjwa yatakayoshughulikiwa ni ya upasuaji,dawa za usingizi, wanawake na watoto na masuala ya uzazi huku Magonjwa mengine ni shinikizo la damu,kisukari, magonjwa ya moyo,macho  na mengineyo.


Sambamba na hilo amesema hakutakuwa na gharama za kuwaona madaktari hao za nyongeza bali ni gharama,zilizoelekezwa na Serikali za kumuona daktari bingwa yoyote.


Mkuu wa Mkoa Queen Sendiga amebainisha kuwa kwa jitihada hizo za Mkoa wa Manyara Serikali na Wizara wataweza kutoa kipaumbele cha kuongeza Madaktari Bingwa  na wabobezi katika magonjwa mengine.


Naye,Mganga Mkuu Mkoa wa Manyara Andrew Method amewahimiza wanawake kuhudhuria kliniki kupata ushauri wa madaktari ili kujiepusha na  magonjwa yanayopelekea vifo vya wajawazito ikiwemo kifafa cha Mimba.

No comments: