MKUU WA WILAYA MOROGORO APIGA MARUFUKU UWEKEZAJI KWENYE VYANZO VYA MAJI - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Wednesday, 6 November 2024

MKUU WA WILAYA MOROGORO APIGA MARUFUKU UWEKEZAJI KWENYE VYANZO VYA MAJI





Na Lilian Kasenene, Morogoro


maipacarusha20@gmail.com


MKUU wa Wilaya ya Morogoro, Mussa Kilakala amepiga marufuku wananchi wa Wilaya hiyo kuendesha shughuli za binadamu na kuwekeza kwenye vyanzo vya maji wakitegemea kulipwa fidia kwamba serikali haitatoa fidia kwao.


Kilakala alitoa rai hiyo wakati akifungua mkutano wa Jukwaa la wadau wa Kidakio cha Ruvu uliofanyika mjini Morogoro.


Aliongeza kuwa wadau hao wanajukumu la kulinda vyanzo vya maji ili binadamu, mifugo na mimea iweze kunufaika na huduma ya maji.


Kilakala alisema kuwa wakazi wa Morogoro wanapaswa kuungana na mamlaka husika,Bonde la Wami Ruvu katika kusimamia na kutunza vyanzo vya maji hasa katika kidakio cha Ruvu. 


Alisema kuwa wapo watu wachache wamekuwa wakiathiri vyanzo hivyo vya maji kwa kujua au  kutojua na kwamba wajumbe wa mkutano huo wanawajibu wa kulinda na kuhifadhi vyanzo vya maji kwa kuweka mpango mkakati na mpango kazi utakaotumika kama vyenzo na kitendea kazi ili kuleta tija.


“Vyanzo vya Morogoro na vilivyopo nje ya Morogoro,ambavyo Wami Ruvu wanavisimamia, ndugu zangu tuna changamoto kubwa sana ya kulinda na kuhifadhi vyanzo vya maji,si jukumu la bonde pekee yao,wala si jukumu la serikali la serikali pekee yao,ni jukumu la watanzania wote kulinda na kutunza vyanzo vya maji.”alisema


Morogoro inaongoza kuwa na vyanzo vingi vya maji ambavyo vinachangia mto Ruvu unaotegemewa kuwahudumia wakazi wa Mikoa ya Morogoro, Pwani na Dar kwamba ili vyanzo hivyo viwe endelevu wadau wanapaswa kuunganisha nguvu ya pamoja katika kulinda na kuvitunza.


Aidha alisema katika safu ya milima ya uluguru wananchi wanakasumba ya kupenda kuwasha moto kwa sababu ya kuandaa mashamba na wengine kwa ajili ya uchomaji wa mkaa bila ya kujali wanaathiri vyanzo vya maji kwamba wadau wanapaswa kuungana na serikali katika kupiga vita vitendo hivyo.


Alipongeza bonde la Wami Ruvu kwa kupanda miti kwenye maeneo yenye vyanzo vya maji,miti ya matunda na mikarafuu ambao ni moja ya uamuzi sahihi ya kuwashirikisha wananchi kuongeza hamasa ya kutunza vyanzo vya maji huku wakipata tija ya kuwa na mazao yanayoweza kuwaongezea kipato.


Sanjari na hilo,Kilakala alisema kuwa kiasi cha shilingi bil.2.5 zimetumika katika ujenzi wa mabirika ya kunyweshea mifugo katika mikoa ya Morogoro na Pwani ili kupunguza migogoro iliyo ya lazima kwa mifugo kuingia kwenye vyanzo vya maji na kuharibifu miundombinu ya vyanzo vya maji.


Alitoa wito kwa viongozi wa wafugaji wa mikoa ya Morogoro na Pwani kuwaelimisha wafugaji wenzao namna bora ya kupunguza mifugo ili kujenga mabirika yatakayosaidia kunywesha mifugo maji.


Alisema kuwa iwapo vyanzo vya maji havitalindwa na kutunza kuna uwezekano mkubwa kwa siku zijazo kwa baadhi ya maeneo kuwa jangwa,kwamba wakazi wa Morogoro wanawajibu wa kulinda bwawa la kidunda ambalo litakapokamilika litaondoa tatizo la maji katika mikoa ya Morogoro, Pwani na Dar es Salaam.


Kuhusu watu wanaochenjua madini kundi hili linahitajika kupewe elimu ya utunzaji wa mazingira kwa kuwa kuna mazingira ya utoaji wa kibali bila ya kujua eneo hilo husika lina chanzo cha maji.


Kwa upande wake,Mkurugenzi wa Bodi ya Maji Bonde la Wami/Ruvu Mhandisi Elibariki Mmassy alisema katika eneo la mto ruvu waliweka mipaka ili shughuli za kibidamu zinapopaswa kuishia kutokana na kuwepo kwa matukio ya uchafuzi wa maji kandokando ya mto.


Mhandisi Mmassy alisema kuwa Wilaya ya Morogoro ina mifugo zaidi ya 20,000,10,000 hadi  15,000  eneo la Mlandizi hadi Bagamoyo mkoani Pwani kutokana na kupitishwa kwa mifugo kulikuwa na migogoro ya mara kwa mara ambapo ng’ombe wanapita kwa kipindi kirefu wanatengeneza korongo na mvua inaponyesha mto unajaa mchanga na kupoteza mwelekeo na kusababisha mafuriko.


“Hatua tuliochukua ni kuchimba kisima na kuweka sola ambayo inasaidia kusukuma maji na kusaidia kunywesha mifugo,pia tumepanda miti katika safu ya milima ya uluguru ili kurudisha uoto wa ajili kwa kuwahamasisha wananchi kupata mikarafu na miparachichi ambayo ina tija kwao,”alisema.


Alisema kuwa Bonde la Wami Ruvu wamejenga mradi wa usambazaji wa maji takriban bil 2 maeneo ya Dakawa,Mngazi kwamba jamii inapotumia maji ardhini katika uchimbaji wa visima yanapaswa kuzingatia upatikanaji wa vibali.


Pamella Temu,ni Kaimu Mkurugenzi,chini ya Idara ya rasilimali ya maji,Wizara ya Maji alisema kuwa uzinduzi wa jukwaa la wadau ya sekta mtambuka ya rasilimali maji katika kidakio cha Ruvu ikiwa ni kutimiza takwa la kisheria linalotaka kuwepo kwa njia shirikishi kwa kuzingatia kanuni na sheria.


Temu alisema kuwa kanuni na sheria ya maji  zinazosimamia rasilimali za maji zinataka kuwepo kwa hatua za kuwashirikisha wadau katika ngazi zote katika kupanga,na kufanya maamuzi katika usambazaji wa rasilimali za maji zinatekelezwa kwa kuzingatia majukumu ya jukwaa la kidakio cha Ruvu yanatekelezwa.


Mkutano wa Jukwaa la wadau kidakio cha Ruvu limewashirikisha wadau mbalimbali kutoka Wilaya za Chalinze, Kisarawe,Bagamoyo na Morogoro ambao ni wenyeji na wanatarajia kupata uongozi mpya ambao utakaa madarakani kwa kipindi cha miaka 3.


Mwisho.

No comments: