THRDC waridhishwa na MAIPAC wanavyotetea haki za jamii za pembezoni - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Wednesday, 6 November 2024

THRDC waridhishwa na MAIPAC wanavyotetea haki za jamii za pembezoni

       



        
KATIKA picha ya pamoja ni Mratibu wa Kitaifa wa THRDC wakili Onesmo Olengurumwa kushoto, Andrea Ashery Ngobole katikati pamoja na Lisa Kagaruki walipotembelea ofisi za maipac mapema jana

Meneja Utawala na Fedha wa Maipac Andrea Ashery Ngobole akiwaeleza maafisa wa THRDC changamoto na utendaji kazi wa utetezi wa Haki kwa jamii za pembezoni zinazofanywa na shirika la MAIPAC 




Na: Mwandishi Wetu, Maipac 


maipacarusha20@gmail.com 


Mtandao wa watetezi wa Haki za binadamu Nchini Tanzania (THRDC), imeeleza kufurahishwa na utetezi wa Haki za jamii za pembezoni unaotekelezwa na shirika la wanahabari la usaidizi wa jamii za Pembezoni ( MAIPAC)


Mratibu wa Kitaifa wa THRDC wakili Onesmo Olengurumwa ametoa pongezi hizo alipotembelea Ofisi ya Maipac kuona shughuli za utetezi wa jamii za pembezoni zinazofanywa na shirika hilo na miradi ambayo inatekelezwa.

Amesema jamii za pembezoni zina changamoto nyingi ambazo hazisikiki, hivyo MAIPAC ina jukumu la kuhakikisha haki zao zinafahamika kupitia vyombo vya habari nchini.


"Mnafanya kazi nzuri ya kutetea haki za jamii hizi kupitia vyombo vya habari, jitahidini kufikia jamii kubwa zaidi ili changamoto zao zijulikane na zipatiwe ufumbuzi." alisema Olengurumwa.  


Alitaka MAIPAC kuendelea na miradi yake ya uhifadhi wa mazingira na kupambana na ukatili dhidi ya wanawake na watoto kwani Kuna changamoto kubwa za ukiikaji wa haki za makundi hayo kwa jamii za pembezoni.

 

Awali meneja wa Utawala na fedha wa MAIPAC Andrea Ngobole alisema taasisi ya Maipac pamoja na changamoto za kifedha inayokumbana nazo  imejitahidi kuhakikisha haki za jamii za pembezoni zinaandikwa katika vyombo vya habari ili kusaidia utetezi wa Haki za binadamu kwa jamii hizo.

Amebainisha haki wanazozipazia sauti kupitia vyombo vya habari ni kupinga ndoa za utotoni na matumizi sahihi ya maarifa ya asili yanayokabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi. 

Ngobole Alisema hadi sasa MAIPAC inaendesha mradi wa uhifadhi wa mazingira na kurekodi maarifa ya asili  katika uhifadhi mradi ambao unafadhiliwa na mfuko wa mazingira duniani (GEF) kupitia Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa(UNDP).

 Alisema pia MAIPAC inaendesha mradi wa kupaza sauti kupinga ukeketaji wilaya ya Longido ambao unafadhiliwa na shirika la marekani la Cultural Survival.  

Alisema pia wanaendelea na mazungumzo na Taasisi kadhaa kuwa na mradi wa matumizi ya nishati safi na salama kwa jamii za pembezoni.

 "Lakini pia tunakusudia kuwa na mradi wa kutengeneza mkaa mbadala ambao ni rafiki kwa mazingira." Alisema

Akizungumzia changamoto Ngobole pia aliomba usaidizi katika kuimarisha mifumo ya  TEHAMA lakini pia kuweza kupata miradi ambayo italiondoa shirika kutegemea wafadhili wa nje pekee. 

Mwisho

No comments: