MOUNT MERU HOSPITAL KUTOA MATIBABU YA KIBINGWA BURE KATIKA KUADHIMISHA MIAKA 63 YA UHURU WA TANZANIA - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Tuesday, 26 November 2024

MOUNT MERU HOSPITAL KUTOA MATIBABU YA KIBINGWA BURE KATIKA KUADHIMISHA MIAKA 63 YA UHURU WA TANZANIA

 


Na: Mwandishi Wetu 


maipacarusha20@gmail.com 


Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Arusha Mount Meru inatarajia kufanya kambi ya madaktari bingwa bure kwa wananchi wa mkoa wa Arusha na maeneo jirani ambapo kambi hiyo itafanyika kwa siku nne mfululizo kwa lengo la kuadhimisha miaka 63 ya Uhuru wa Tanzania bara.


Akizungumza kupitia vipindi mbalimbali vya radio leo hii Mganga mfawidhi wa hospitali ya Mount Meru, Dkt. Alex Ernest amesema kuwa kambi hiyo ya matibabu itatoa matibabu bure kwa wananchi wa mkoa wa Arusha na wale wananchi wanaotoka katika mikoa mingine na huduma za vipimo, dawa Pamoja na matibabu ya kibingwa vitatolewa bure.


“kambi hii ya madaktari bingwa itatoa huduma za kimatibabu bure kwa wananchi wa mkoa wa arusha na maeneo Jirani hivyo niwahakikishie kuwa zaidi ya madaktari bingwa 28 watashiriki kuwapa huduma bure wananchi wote watakaofika katika viwanja vya hospitali ya Mount Meru kwa siku zote nne za kambi watapata huduma nzuri zikiwepo huduma za  vipimo,dawa Pamoja na matibabu bure kabisa”.Amesema Dkt. Alex Ernest


Dkt. Alex amesema kuwa kambi hiyo ya madaktari bingwa itaanza rasmi tarehe 06/12/2024 hadi tarehe 09/12/2024 siku ya kilele cha maadhimisho ya siku ya Uhuru wa Tanzania bara na amewataka wananchi wote wenye changamoto za kiafya kufika na  kuchunguza afya zao bure ikiwa ni Pamoja na kupata matibabu bure.


Naye Dkt. Edward Feksi ambaye ni Daktari bingwa wa radiolojia amesema kuwa katika kuadhimisha miaka 63 ya uhuru wa Tanzania wapo tayari kuwahudumia wananchi bure kwa kuwapa huduma za vipimo,dawa Pamoja na matibabu wananchi wote watakaofika katika kambi hiyo ya mdaktari bingwa.


Kwa upande wake Dkt. Emmanuel Kinai ambae ni daktari bingwa wa magonjwa ya ndani amesema kuwa watumishi wote wapo tayari kuwahudumia wananchi bure katika kipindi chote cha kambi ya madaktari bingwa kuelekea katika maadhimisho ya miaka 63 ya uhuru wa Tanzania.


Katika kambi hii ya madaktari bingwa, zaidi ya madaktari bingwa 28 kutoka Nyanja mbalimbali wanatarajiwa kushiriki kuwahudumia wananchi wa mkoa wa Arusha na maeneo Jirani bure kwa kufanya vipimo, kuwapatia dawa Pamoja na kuwapa matibabu ya kibingwa bure.

No comments: