Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro SACP Alex Mkama
Na: Lilian Kasenene, Morogoro
maipacarusha20@gmail.com
MWANAMKE aliyefahamika kwa jina la Subira John (25) mkulima mkazi wa Mtendeni Wilaya ya Kilosa anashikuliwa na Polisi mkoani Morogoro kwa kosa la kutelekeza kichanga cha siku moja kikiwa hai.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro SACP Alex Mkama alisema tukio hilo limetokea Novemba 8,2024 majira ya mchana katika eneo la K Park bar kitongoji cha Mbumi Kata ya Mbumi Wilaya ya kilosa.
SACP Mkama alisema mtuhumiwa huyo alikifukia kichanga hicho chenye umri wa siku moja jinsia ya kiume na kuacha kichwa nje ya shimo na kutoroka kusikojulikana.
Ikumbukwe kuwa Novemba 8, 2024 kupitia mitandao ya Kijamii zilisambaa taarifa za utelekezwaji wa kichanga hicho na Jeshi la Polisi lilianza uchunguzi ili kubaini mtuhumiwa wa tukio hilo.
Baada ya ufuatiliaji Disemba 2, 2024 Polisi ilimkamata mtuhumiwa akiwa kajificha kwenye nyumba ya wageni isiyo na jina maarufu (Gesti bubu).
Aidha jeshi la Polisi kwa kushirikiana na taasisi nyingine ikiwemo Ustawi wa jamii lilifanikiwa kukichukua kuchanga hicho na kukipeleka katika kituo cha kulelea watoto Mgolole kilichopo kata ya Bigwa Manispaa ya Morogoro na kwasasa kichanga hicho kinaendelea vizuri.
Kamanda Mkama alisema upelelezi unaendelea kukamilishwa kwa ajili ya hatua nyingine za kisheria.
Pia Jeshi hilo la Polisi linatoa wito kwa wananchi kuacha tabia ya kutelekeza vichanga na badala yake wavilee kwani hilo ni taifa la kesho.
.....
No comments:
Post a Comment