Na: Mussa Juma,maipac
maipacarusha@gmail.com
Wakazi wa jiji la Arusha, wamesherehekea kuzaliwa kwa Rais Samia Suluhu kwa aina yake ikiwepo kutoa misaada kwa watoto wanaoishi kwenye mazingira magumu, walemavu na watoto yatima.
Maadhimisho ya kuzaliwa Rais Samia yaliratibiwa na taasisi ya Suluhu Foundation na kukusanya mamia ya wakazi wa Arusha wakiwepo watoto, makada wa CCM na viongozi wa dini.
Katika maadhimisho hayo mgeni rasmi alikuwa meya wa jiji la Arusha, Maxmillian Matle Irange akiwa pamoja na makada kadhaa wa CCM na viongozi wa serikali.
Akizungumza wakati akikata keki na watoto wanaoishi katika mazingira Magumu Meya Irange aliwataka wakazi wa Arusha kuendelea kumuunga mkono Rais Samia Suluhu .
"Leo tunasherehekea siku ya Rais wetu kuzaliwa na tunampongeza Sana Rais kwa kazi kubwa ambayo anaifanya kuwaletea maendeleo watanzania"alisema
Alisema kutokana na kazi nzuri ya Rais Samia ndio sababu CCM imempitisha tena kuwa mgombea urais katika uchaguzi mkuu ujao.
Mratibu wa maadhinisho hayo, Athumani Singano alisema lengo la kusaidia watoto wenye ulemavu wa ngozi na wanaoishi kwenye mazingira magumu kufurahi.
"Rais Samia anawapenda watu wote ndio leo tunafurahi na watoto wenye ulemavu wa ngozi na watoto wanaosoma katika kituo cha Madrasati Hidaya"alisema
Katika maadhimisho hayo Meya wa jiji na viongozi pia walitembelea ujenzi wa msikiti wa kisasa wa Hidaya ambapo Sheikh wa msikiti huo sheik Omary Said licha ya kumshukuru Mungu kwa kumleta Rais Samia pia aliomba wadau mbalimbali kujitokeza kuchangia ujenzi wa msikiti huo.
Sheikh Omar aliongoza pia dua ya kumtakia kheri na baraka Rais Samia lakini pia kumkinga na maadui .
Katika maadhimisho hayo, watoto na wakazi wa Arusha waliohudhuria walitangaza kumuunga mkono Rais Samia katika uchaguzi ujao .
Mwisho
No comments:
Post a Comment