Na Epifania Magingo,Manyara
maipacarusha20@gmail.com
Mkuu wa Wilaya ya Babati, Emmanuela Mtatifikolo Kaganda,amefanya kikao na baadhi ya wawekezaji wa kilimo katika Wilaya ya Babati ili kusikiliza changamoto zinazowakabili na kuweka mikakati ya kuboresha mazingira ya uwekezaji.
Katika kikao hicho, usalama wa wawekezaji ulitajwa kuwa changamoto kubwa, hali inayowafanya washindwe kutulia na kuendesha shughuli za uzalishaji kwa ufanisi.
Baadhi yao wameleza kuwa ukosefu wa ushirikiano na wananchi wanaozunguka mashamba yao umesababisha migogoro inayosababisha vurugu na uvamizi wa maeneo yao, jambo linalohatarisha maendeleo ya sekta ya kilimo.
Aidha, wawekezaji wamesema uharibifu wa mazingira unaosababishwa na ukataji miti holela katika misitu inayozunguka mashamba yao umekuwa tishio kwa ustawi wa kilimo.
Wamema baadhi ya wananchi wamekuwa wakivamia mashamba yao kwa ajili ya kuchoma mkaa na kufanya uharibifu mkubwa wa mazingira, hali inayosababisha mmomonyoko wa ardhi na upungufu wa rutuba.
Kwa upande wake, Kaganda, amewahakikishia wawekezaji hao kuwa Serikali itasimamia usalama wao ili kuhakikisha uzalishaji unaongezeka.
Ameahidi kuwa maeneo yote yenye changamoto ya uvamizi yatapewa utaratibu rasmi wa utatuzi, na iwapo vitendo vya vurugu vitaendelea, hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya wahusika.
Kaganda pia amemuelekeza Afisa wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS)kusimamia mazingira kwa ukaribu na kuhakikisha sheria zinachukuliwa kwa wale wote wanaochoma mkaa au kufanya uharibifu wa misitu.
Katika hatua nyingine, wawekezaji na wadau wa kilimo wamependekeza hatua mbalimbali za kuimarisha amani na ufanisi wa uwekezaji wao, ikiwemo kuongeza vituo vya polisi katika maeneo yenye changamoto za kiusalama na kutoa elimu kwa wananchi kuhusu ufugaji wa kisasa na wenye tija ili kupunguza idadi ya mifugo isiyo na faida.
No comments:
Post a Comment