Na: Epifania Magingo,Manyara
maipacarusha20@gmail.com
Siku chache tangu kuanza kwa muhula mpya wa Masomo 2025 baadhi ya watoto Wilayani Babati wanatajwa kushindwa kuhudhuria masomo kutokana na kukosa mahitaji muhimu ya Shule ikiwemo sare na madaftari hivyo jamii yenye uwezo umeombwa kujitokeza kuchangia mahitaji hayo kupitia kampeni ya MLINDE ASOME.
Kampeni hiyo ya Mlinde Asome inaendeshwa chini ya wadau wa maendeleo wanaounga mkono juhudi za Serikali katika kukuza na kuifikia jamii yote kielimu ambapo misaada ya mahitaji hayo ya shule yatapokelewa katika Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Babati.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni hiyo uliofanyika Januari 15, 2025, Kaganda amewahimiza wananchi kutoa ushirikiano huku akisisitiza umuhimu wa jamii kuhakikisha watoto wote wanapata nafasi ya kutimiza ndoto zao kupitia elimu.
Amebainisha kuwa Serikali imeweka mazingira mazuri kwa elimu, lakini akawataka wazazi na walezi kutimiza wajibu wao wa kuwapatia watoto mahitaji muhimu ya shule.
"Maelekezo ni kwamba watoto wote waliofikia Muda wa kwenda shule wapelekwe shule,ada imeshalipwa na Serikali wazazi hawana mzigo Tena,kwa watoto ambao hawana Sare au mahitaji waje tu shuleni wakati jitihada zikiendelea kufanyika" .Kaganda amesema
Katika hafla hiyo, Kaganda alikabidhi sare za shule na madaftari kwa baadhi ya wanafunzi na pia ameelezea kuwa hatua hii ni mwanzo wa juhudi za kuboresha maisha ya watoto wengi zaidi kupitia elimu.
Kwa upande wake,Lucas Mondu, Mkurugenzi wa Mr. Faida Brand, amesema kampeni hiyo inalenga kuwasaidia watoto zaidi ya 200 katika Wilaya ya Babati, huku shule za msingi zikipewa kipaumbele katika awamu za kwanza za utekelezaji.
Mratibu wa kampeni, Alphonsina Andrew, amefafanua kuwa gharama ya kumsaidia mwanafunzi mmoja ni shilingi 25,000 na akatoa wito kwa jamii kushiriki kuchangia ili kufanikisha malengo ya kampeni.
Wazazi na wanafunzi walionufaika wameonyesha furaha na shukrani zao,ambapo baadhi ya wanafunzi wameeleza kuwa msaada huo umewapa matumaini mapya ya kufanikisha masomo yao.
"Sasa nitasoma kwa furaha na amani, nashukuru kwa zawadi hii,nimepata sketi,Sweta,shati , madaftari na kamalu".Noela Daud amesema
No comments:
Post a Comment