Mhasibu afikishwa mahakamani, asomewa mashtaka 52 ya Utakatishaji wa Fedha - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Friday, 24 January 2025

Mhasibu afikishwa mahakamani, asomewa mashtaka 52 ya Utakatishaji wa Fedha




Na Epifania Magingo, Manyara 


maipacarusha20@gmail.com 


Mhasibu Msaidizi wa Zahanati ya Endanachani Mohamed Baya(33) mkazi wa Babati Wilayani Babati Mkoani Manyara amefikishwa mahakamani na kusomewa mashtaka 52 ya ubadhirifu na ufujaji, utakatishaji fedha haramu pamoja na kughushi ambao umessababisha upotevu wa fedha kiasi Cha Shilingi milioni  48.09.


Baya alifikishwa mahakamani 23 Januari 2025 na kusomewa mashtaka 52 yanayomkabili na wakili wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Martini Makani akisaidiana na Davis Masambu na Catherine Ngesi mbele ya hakimu Mkazi mkuu wa mahakama ya Wilaya ya Babati Karimu Mushi.


Akisoma mashtaka hayo Wakili Makani alisema shtaka la kwanza ni ubadhirifu na ufujaji, shtaka la pili ni utakatishaji fedha haramu na shtaka la tatu ni kughushi.


Aidha, alisema mashtaka mengine 49 yanafanana na shtaka la kughushi kinyume na sheria ya kanuni ya adhabu sura ya 16 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2022.


Mwendesha mashtaka huyo alisema kwa kosa la kwanza mshtakiwa alikiuka sheria ya sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa kifungu cha 28 (1) Aya ya 21 jedwali 1 kifungu cha 57(1) na 60(2) vya sheria ya uhujumu uchumi na makosa ya kupanga sura 200 kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2022.


Alieleza kuwa Baya, Oktoba 17 mwaka 2022 akiwa Halmashauri ya wilaya ya Babati mkoani Manyara katika Zahanati ya Endanachan akijua na kwa makusudi aliandaa nyaraka za hundi Oktoba 17 mwaka 2022  kwa lengo la kuonesha nyaraka zimesainiwa na watia saini ili kwenda kutoa Mil. 1.5 Benki akiamini nyaraka ziko sahihi.


Makani alisema mshtakiwa huyo akiwa na nyaraka zisizo halali aliandaa hundi yenye namba 000182 Septemba 17 mwaka 2022 na kutoa  Mil. 1.2 Benki bila kujali nyaraka zake siyo sahihi.


Alisema mshtakiwa huyo aliendelea kughushi nyaraka kwa nyakati tofauti na kutoa fedha kinyume na utaratibu hatimaye kufikia viwango cha Mil. 48.09.


Mwanasheria huyo wa TAKUKURU aliieleza mahakama kuwa upelelezi wa shauri hilo namba 2081 la mwaka huu la uhujumu uchumi umekamilika na aliomba shauri hilo lipangwe ndani ya siku 14 ili kusikiliza hoja za awali.


Alitumia fursa hiyo kuiomba mahakama isitoe dhamana kwa mshtakiwa kwa kesi ya uhujumu uchumi haina dhamana.


Baada ya kusomewa mashtaka Baya alikana mashtaka yote 52 yanayomkabili na Hakimu Mushi aliairisha kesi mpaka Februari 5 mwaka huu kwa ajili ya kusikilizwa.


Mushi alisema mshtakiwa ataendelea kukaa lumande kwa kuwa makosa mawili ya utakatishaji fedha hayaruhusu kupata dhamana.

No comments: