Na Lilian Kasenene,Morogoro
maipacarusha20@gmail.com
RAIS mstaafu Jakaya Kikwete ametahadharisha watu kutotumia mwamvuli wa dini kueneza chuki katika jamii hali ambayo inaweza kusababisha machafuko,
Aidha amewataka viongozi wa dini kusimama imara na kuhakikisha Tanzania inaendelea kuwa kisiwa cha amani, utulivu na umoja sambamba na kusimamia Maadili kwa vijana Tanzania.
Rais Huyo mstaafu wa awamu ya nne alisema hayo mkoani Morogoro wakati wa kikao cha kamati kuu cha Jumuiya ya maridhiano na Amani Tanzania (JMAT) .
Kikwete aliitaka taasisi hiyo ya (JMAT) kuendelea kutatua migogoro ya wakulima na wafugaji ambapo alisema tangu kuanzishwa kwa taasisi hiyo mwaka 2015 migogoro hiyo imepungua.
"Amani na utulivu havinunuliwi, sisi Watanzania ni wa moja, hatuna sababu ya kubaguana kwa imani za dini, rangi wala ukabila,"alisisitiza.
Kuhusu maadili kwa vijana aliwataka kuhakikisha wanaongeza nguvu ili vijana wa Tanzania wanaishi katika mila na desturi za Tanzania.
"Bado kuna changamoto kwenye malezi, maadili ni jambo la muhimu kulisimamia ili vijana wetu wasiharibike na utandawazi," alisema.
Katika hatua nyingine Kikwete alikemea baadhi ya vyombo vya habari vinavyotumika kuchochea uvunjifu wa amani na kwamba havitavumilika.
"Mimi ni muumini mkubwa wa Uhuru wa habari lakini uhuru ni ule unaojenga na sio kubomoa," alisema.
Mwenyekiti wa JMAT Alhaji Dk Mussa Salim alisema taasisi hiyo haina lengo la kufanya ibada za dini mseto kama baadhi ya watu wasikokuwa na nia njema wanavyofikiria nakwamba kinachofanyika ni kutafuta amani na utulivu wa nchi huku kila dini ikiabudu kwa imani yake.
"Hiki sio chombo cha kidini bali kinaongozwa na viongozi wa dini na hatujawahi kufanya dini mseto na hilo haliwezekani katika madhahebu yote"alisema.
Aliwahimiza viongozi wa dini kufanya matendo mema kwani wao wanafananishwa na chumvi ambayo ni kiungo muhimu ambayo ikichafuka haiwezi kusafishwa na kitu chochote.
Naye mkuu wa mkoa wa Morogoro Adam Malima alisema mkoa wa Morogoro miaka ya zamani ulikuwa ukisifika kwa migogoro ya Ardhi na wakulima na wafugaji ambapo tangu kuanzishwa kwa taasisi hiyo sifa hiyo haipo tena.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment