Na Lilian Kasenene, Morogoro
maipacarusha20@gmail.com
WAKATI Rais Samia Suluhu Hassan akitarajiwa kuzindua Sera mpya ya Elimu na mafunzo ya Mwaka 2014 Toleo la Mwaka 2023, Baraza la Taifa la elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi (NACTVET) imeeleza kuwa itapokea na kuyaendeleza malengo makubwa saba yaliyopo kwenye sera hiyo.
Kaimu katibu mtendaji wa Baraza hilo la NACTVET Dk Amani Makota alieleza hayo mjini Morogoro wakati akizungumza na vyombo vya habari mara baada ya kumalizika kwa mafunzo ya kujengeana uelewa kuhusu majukumu ya ubora wa mafunzo hasa kwenye mafunzo ya Amali kwa wafanyakazi wa NACTVET..
Dk Makota alisema NACTVET kama taasisi imejipanga kupokea Sera hiyo kwa sababu ndani ya malengo saba, NACTVET ina malengo matatu(3) ya kufanyia kazi lakini kubwa zaidi likiwa ni utekelezaji wa mafunzo ya Amali.
"Baada ya kutoka kuwa Nacte Sasa tumeenda Nactvet tunaendelea kukumbushana ni namna gani ya kutekeleza, kushirikiana na kushauriana na Serikali kwenye majukumu,"alisema Dk Makota.
Aidha alisema kwa Sasa Nactvet imeanza kufanyia kazi yale maeneo yote yanayowahusu lakini pia wataendelea kukutana na jinsi kutekeleza majukumu yao.
Akizungumza wakati wa mafunzo hayo, mwenyekiti wa Baraza la Uongozi la NACTVET Bernadeta Ndunguru alisema kuna umuhimu wa Wizara ya Elimu na sekta zake kukaa pamoja kuelezana, kujadili mambo mbalimbali kwa nia ya kujenga kwa manufaa ya watanzania.
Ndunguru alisema kama Baraza la Uongozi ni vyema wakakasimu baadhi ya majukumu kwa kuwachukua wataalamu ambao Wana uzoefu kwa baadhi ya maeneo, huku aliwataka wafanyakazi wa taasisi hiyo ya Nactvet kufanyakazi kwa mwendo wa kukimbia na si kutambaa ili kuendana na Kasi ya Sasa.
Mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo, Elita Mbedule alisema kwa Sasa mafunzo yamewafanya kufahamu majukumu yao hasa kwenye suala zima la usimamizi na kwamba wanachotakiwa ni kuangalia maeneo ya kuboresha na kuzitembelea shule katika kuhakikisha zinatekeleza mitaala kama ilivyotarajiwa nakuwa na walimu.
Alisema maeneo mengine ni kuwepo kwa vifaa vinavyotakiwa kutumika ili wahitimu wawe na umahili unaotakiwa kwenda kufanyakazi au kujiajiri wenyewe.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment