Na Mwandishi wetu, Kiteto
maipacarusha20@gmail.com
MKUU wa Mkoa wa Manyara, Queen Cuthbert Sendiga amempongeza Mbunge wa Jimbo la Kiteto Wakili msomi Edward Ole Lekaita Kisau kwa namna anavyowaongoza vyema wakazi wa eneo hilo.
Sendiga akizungumza na wakazi wa kijiji cha Njoro Wilayani Kiteto amesema Ole Lekaita ni mbunge mahiri mwenye kujitambua na anayetekeleza vyema wajibu wake.
Amesema japokuwa mbunge huyo ana asili ya jamii ya wafugaji ila kwenye uongozi wake hana ubaguzi kwa kuwapendelea wafugaji wala kuwanyanyasa wakulima.
Amesema mbunge huyo amefanya kazi kubwa mno hivyo watu wa Kiteto wanapaswa kumshika mkono kwani ni aina ya viongozi wanaowataka.
'Simpigii kampeni ila kesho kutwa ntawashangaa sana mkimuacha kwani ni mbunge mwenye kujitolea kwa moyo mmoja katika kuwatumikia vyema wananchi wake bila kuwachonganisha na serikali," amesema RC Sendiga.
Amesema Ole Lekaita amesimama katikati bila kujali lolote na amekuwa akisimamia ukweli kwani ardhi ikitengwa kwa ajili ya kilimo anasema hii ni kwa kilimo na inayotengwa kwa ufugaji anasema ni ya ufugaji.
"Utulivu unaoendelea kwenye wilaya yetu ya Kiteto umetokana na hisani ya ushirikiano mkubwa wa mbunge na viongozi wa serikali ambao kila jambo wanalifanya kwa pamoja," amesema RC Sendiga.
Amesema tangu afike Kiteto hajawahi kuwaeleza hayo wananchi wa Kiteto ila anayazungumza kwa dhati ya moyo wake kutokana na utendaji kazi bora wa Ole Lekaita.
Kwa upande wake mbunge huyo Ole Lekaita amemshukuru RC Sendiga kwa kutambua juhudi zake katika kuwaongoza wana Kiteto.
MWISHO
No comments:
Post a Comment