MAHAKAMA YA TANZANIA, KIWANGO CHA UMALIZAJI MASHAURI CHAONGEZEKA KWA ASILIMIA 101 - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Thursday, 6 February 2025

MAHAKAMA YA TANZANIA, KIWANGO CHA UMALIZAJI MASHAURI CHAONGEZEKA KWA ASILIMIA 101

 




Na Lilian Kasenene, Morogoro 


maipacarusha20@gmail.com


MAHAKAMA ya Tanzania imesema kiwango cha umalizaji wa mashauri kimeongezeka kwa asilimia 101, na  kiwango cha uondoshaji wa mashauri kikipanda kwa asilimia 84 na wastani wa muda wa kumaliza shauri ukipungua hadi siku 78.


Mtendaji Mkuu wa Mahakama nchini,  Profesa Elisante Ole Gabriel alisema hayo mjini Morogoro wakati akizungumza  kuhusu utekelezaji wa bajeti na majukumu ya Mahakama ya Tanzania kwa nusu mwaka wa fedha 2024/2025.


Profesa  Ole Gabrial alisema kuwa Mahakama ya Tanzania imeendelea kutekeleza jukumu lake la kikatiba la utoaji haki kwa Wananchi kwa ufanisi mkubwa kwa mwaka 2024.


“  Mahakama imepiga hatua katika viashiria vyote vikuu vya utendaji kazi ikilinganishwa na mwaka 2023”alisema Profesa Ole Gabriel .


Profesa Ole Gabriel alisema kuwa Mahakama za Mwanzo ambazo zimehudumia Wananchi wengi zaidi kwa asilimia 70 wanaotafuta haki kwenye mfumo wa Mahakama zilitumia wastani wa siku 37 kumaliza shauri moja.


Mtendaji Mkuu  alisema ,wastani wa mashauri kwa kila Jopo umepungua toka mashauri 234 mwaka 2023 hadi 227 mwaka 2024.


Alisema kuwa siri ya mafanikio hayo inatokana na utendaji na uwajibikaji nzuri wa Majaji, Mahakimu, Watendaji na Watumishi wa Mahakama kwa ujumla, ushirikiano wa Wadau, matumizi ya teknolojia na uwezeshaji wa Serikali katika maeneo mbalimbali, ikiwemo rasilimali fedha na watu.


Katika kipindi husika, Mtendaji Mkuu amebainisha kuwa jumla Majaji watano wa Mahakama ya Rufani na Jaji mmoja wa Mahakama Kuu ya Tanzania wameteuliwa, hivyo kuongeza kasi ya usikilizaji na umalizaji wa mashauri.


Aidha, Prof. Ole Gabriel amesema, katika kipindi husika, Mahakama ya Tanzania imeajiri jumla ya watumishi 498, kati yao wakiwa Mahakimu Wakazi 88, Watumishi 1,167 wamepandishwa vyeo na wengine 107 wamebadilishwa kada, kati yao wakiwa Mahakimu Wakazi 43.


Pia alisema Mahakama ya Tanzania, katika kutekeleza majukumu yake ya kikatiba, inatumia Mpango Mkakati wa Mwaka 2020/21- 2024/25 ambao umeweka vipaumbele katika maeneo mbalimbali.


Profesa Ole Gabriel aliyataja maeneo hayo ni kuharakisha utatuzi wa mashauri na kutekeleza mkakati wa kumaliza mashauri ya muda mrefu; kuimarisha uwezo katika ukaguzi na usimamizi wa shughuli za Mahakama na kuendelea kutekeleza Mpango wa Ujenzi na Ukarabati wa Majengo ya Mahakama katika ngazi mbalimbali.


Maeneo mengine ni kuboresha Mifumo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kama nyenzo muhimu ya kuboresha utoaji wa huduma; kuongeza ushirikiano na Wadau ili kuharakisha huduma ya utoaji haki na kuimarisha maendeleo ya rasilimaliwatu, ikiwa ni pamoja na mafunzo na nidhamu kwa Watumishi.


Kwa mujibu wa Ibara ya 4(2) na 107A (1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, chombo chenye mamlaka na kauli ya mwisho katika kutekeleza utoaji haki ni Mahakama ya Tanzania. Mahakama ya Tanzania ipo katika ngazi za Mahakama ya Rufani, Mahakama Kuu (Kanda na divisheni), Mahakama za Hakimu Mkazi, Mahakama za Wilaya na Mahakama ya Mwanzo.

..

No comments: