WATERAID KUSAIDIA JAMII HANANG' KUPITIA MRADI WA MAJI - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Monday, 3 February 2025

WATERAID KUSAIDIA JAMII HANANG' KUPITIA MRADI WA MAJI

 





Na Mwandishi wetu, Hanang'


maipacarusha20@gmail.com 


WATERAID inatarajia kufanikisha mradi wa maji safi na salama Wilayani Hanang' Mkoani Manyara, na jamii ya eneo hilo kunufaika na mradi maji kwa asilimia 100 na kuondokana na magonjwa ambukizi yanayotokana na uchafu wa mazingira na vyanzo vya maji.


Mradi huo unatekelezwa na shirika la WaterAid la Uingereza kwa kushirikiana na wakala wa maji na usafi wa mazingira vijijini (RUWASA) mkoani Manyara.


Mkuu wa miradi wa WaterAid Tanzania, Beda  Levira, amesema mradi huo unatarajiwa kukamilika mwezi Agosti mwaka 2025.


Levira amesema WaterAid katika kutekeleza mradi wa mfano Hanang' utatatua changamoto ya maji safi, vyoo bora na usafi wa mazingira na utanufaisha wakazi 368,000 wa vijiji 96 wa kata 33 za wilaya ya Hanang' .


"Watu watapata maji kwa asilimia 100 na kuondokana na changamoto ya magonjwa ambukizi yanayotokana na uchafuzi wa mazingira na vyanzo vya maji," amesema Levira.


Mhandisi wa maji kutoka RUWASA, Barnabas Taligunga amesema mradi huo utaongeza nguvu ya uboreshaji wa usafi wa miundombinu ya kusambaza maji kutoka kwenye vyanzo hadi kwa watumiaji ili kudhibiti uwezekano kusambaa magonjwa kipitia maji. 


"Mradi huu wa mfano kwa hapa Tanzania unafanyika hapa Hanang' pekee hivyo wilaya nyingine zitapaswa kuja kujifunza huku juu ya utekelezaji wa mradi huu," amesema.


Akizungumza kwa niaba ya Katibu Tawala wa Mkoa wa Manyara, mganga mkuu wa mkoa wa huo Dkt Andrew Method ametoa wito kwa viongozi wa Hanang' kutoa ushirikiano wa kutosha kwa WaterAid kutekeleza mradi huo ili uwe mfano kwa wilaya nyingine.


"Pamoja na hayo hatuna budi kumshukuru na kumpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kukubali mradi huu kufanyika huku kwetu Manyara, hususani wilayani Hanang' kwani ni mradi wa mfano," amesema Dk Method.


Mkurugenzi mtendaji na mipango wa kimataifa wa WaterAid, Amaka Godfrey amevutiwa na namna viongozi na jamii ya eneo hilo kwa ujumla walivyoupokea mradi huo na namna walivyojiandaa kushiriki katika kuufanikisha.


Amaka amesema mbinu waliyoichagua viongozi ya kufikia jamii nzima katika wilaya hiyo  ni nzuri kwani itaweza kufikia watu wengi kwa wakati.


Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya hiyo, Rose KamilI amelishukuru shirika hilo kwa kuichagua Hanang' katika kufanikisha mradi huo. 


Kamili ameeleza kwamba ili kuona thamani ya mradi huo wanatarajia kufanikisha zaidi kupitia fedha za mapato yao ya ndani.


Kwa upande wao, baadhi ya wakazi wa wilaya ya Hanang' wamesema kuwa wataulinda mradi huo ili uweze kuwanufaisha wao na kizazi kijacho.


Mmoja kati ya wakazi hao Isack Mayomba amesema wanawashukuru viongozi walifanikisha mradi huo kutekelezwa wilayani Hanang'.


"Mwaka 2023 tulipatwa na matatizo hapa Hanang' na leo 2025 tumepata mradi huu, ni jambo la kumshukuru Mungu kwani amezidi kutufuta machozi," amesema Mayomba.


Mradi huu utakapokamilika, Hanang' itatumika kama mfano kwa wilaya nyingine nchini katika kujifunza.


MWISHO

No comments: