![]() |
Kiongozi wa kambi ya wahadzabe Msafiri Thomas akizungumza changamoto zinazowakabili |
Na: Mwandishu wetu
maipacarusha20@gmail.com
Wananchi wa Jamii ya wahadzabe wanaoishi katika eneo la Eyasi wilayani Karatu Mkoani Arusha, wameiomba serikali kuu kuingilia kati mgogoro wa kuondolewa katika makazi yao ambayo wametunza kwa kutumia maarifa ya asili muda mrefu.
Jamii hiyo imepewa notisi ya siku 14 kuhama katika makazi yao ili kumpisha mfanyabiashara mmoja(jina linahigadhiwa) ambaye ameuziwa ardhi hiyo ili kulima vitunguu.
Wakizungumza na waandishi wa habari katika Kijiji cha Qandet wilaya ya Karatu, waliotembelea eneo hilo kufanya uhakiki wa taarifa za maarifa ya asili ya jamii hiyo katika uhifadhi, mradi unaotekelezwa na taasisi ya wanahabari ya kusaidia jamii za pembezoni (MAIPAC) kwa ufadhili wa mfuko wa mazingira Duniani (GEF) kupitia programu ya miradi midogo ya shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) na Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira jamii hiyo imeomba serikali kuwasaidia.
Katibu wa Wahadzabe eneo la Eyasi, Maria Yona anasema wanaiomba serikali kuwasaidia wasiondolewe kwenye ardhi ya waliyoitunza muda mrefu kwa maarifa ya asili.
Anasema ardhi yao ya asili inaendelea kuvamiwa na wakulima na kusababisha kukosa hadi chakula cha asili, ikiwepo matunda, mizizi na asali.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wahadzabe, Mdindi Samboga alisema jamii ya kihadzabe, inaomba serikali kuwamilikisha ardhi yao kama ilivyo jamii nyingine.
Alisema Wahadzabe wenzao wa Yaeda chini, wilaya ya Mbulu wamepata hati miliki ya kimila za maeneo yao hivyo hawavamiwi sana
Mhadzabe mwingine, Ng’o Nkoo (msafiri Thomas) anasema maisha yao yamekuwa ya shida sana.
Kwani hawana ardhi, chakula, kwa sababu hakuna Wanyama na asali ya kutokana na uvamizi.
Afisa Maendeleo ya jamii kata ya Baray, Kassim Miraji anakiri jamii ya kihadzabe bado inachangamoto ya ardhi ikiwepo mikopo ya wanawake.
Alisema Serikali imetoa fedha za mikopo kwa wanawake na katika eneo hili mimi ndio napaswa kushughulikia ninaahadi kuanzia leo ntaanza kuwasaidia kujiunga katika vikundi ili wanufaike na mikopo.
Mwenyekiti wa bodi ya Utalii katika eneo la Lake Eyasi, Daniel Hhawu anasema ni kweli jamii ya Kihadzabe wakiwepo wanawake wanakabiliwa na shida nyingi licha ya kuwa kivutio cha watalii.
Alisema ni kweli ardhi ya wahadzabe inavamiwa na wanakosa chakula ila mambo haya yapo chini ya serikali sisi kama bodi ya Utalii katika eneo hili hatuhusiki na masuala ya ardhi na kilio chetu tunaomba wasaidiwe
Mkurugenzi wa MAIPAC, Mussa Juma anasema wameamua kuifikia jamii ya Wahadzabe ili kukusanya maarifa yao ya asili katika uhifadhi na kuandaa kitabu.
Awali wanawake wa jamii hiyo walishiriki katika mdahalo wa kujua changamoto zao uliandaliwa na MAIPAC kwa kushirikiana na SAVVY FM na Walieleza pia shida ya ardhi yao kuvamiwa, kukosa maji, chakula cha asili na huduma nyingine muhimu
Wanawake wa jamii hiyo pia waliwezeshwa kufika jijini Arusha kuhudhuria maadhimisho ya siku ya wanawake duniani ambayo mgeni rasmi alikuwa Rais Samia Suluhu.
Mwisho
No comments:
Post a Comment